Wanawake wameathirika zaidi katika utawala wa Taliban
20 Februari 2022Maelfu kwa maelfu ya Waafghanistan wamekimbia au wamehamishwa ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wasomi wakihofia mustakabali wao wa kiuchumi au ukosefu wa uhuru chini ya utawala wa sasa wa kundi la Taliban. Wakati wa utawala wake wa awali mwishoni mwa miaka ya 1990 kundi hilo liliwazuia wasichana kwenda shuleni na wanawake kufanya kazi.
Jumanne (15.02.2022) ilitimia miezi sita tangu mji wa Kabul ulipoangukia mikononi mwa Taliban na kisha ghafla kuondoka kimya kimya rais wa zamani wa nchi hiyo Ashraf Ghani aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani.
Kudhibitiwa mji mkuu Kabul kulitanguliwa na operesheni kubwa za miezi kadhaa za kijeshi zilizofanywa na kundi hilo la Taliban na kuyatwaa maeneo chungu nzima ya mikoa ya nchi hiyo, ambapo mingi ya mikoa hiyo ilidhibitiwa na Taliban hata bila ya kushuhudiwa mapambano.
Hata hivyo hadi sasa wapiganaji wa Taliban waliojihami na silaha wanaonekana wakizunguka mitaani na hali hiyo inawatia hofu wakaazi. Lakini pamoja na hilo wanawake wamerudi mitaani na vijana wengi wa kiume wakionekana tena kuanza kuvaa mavazi ya kimagharibi. Huko nyuma walazimishwa kuvaa mavazi ya kiasili ya Kiafghani, ambayo ni kanzu na suruali au Shalwar Kameez kama wanavyoita wenyewe, mavazi ambayo yanapendelewa zaidi na Taliban.
Maelfu ya ajira zimepotea kutokana na hali ya kudorora kwa uchumi na wanawake wameathirika zaidi.
Taliban na mustakabali wa wanawake
Taliban wamedhibiti maandamano ya wanawake na kuwanyanyasa waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na kuwashikilia kizuizini kwa muda mfupi waandishi wa habari wawili wa kigeni wanaofanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wiki iliyopita.
Jumatatu kuzuiliwa kwa baadhi ya vijana wadogo wanaouza maua yenye umbo la moyo katika kutambua Siku ya Wapendanao kulikuwa ni ukumbusho kamili kwamba utawala mpya unaohodhiwa na wanaume na wenye mwelekeo wa msimamo mkali hauna uvumilivu na mawazo ya kimagharibi ya mapenzi.
Wasichana wa darasa la kwanza hadi la sita wamekuwa wakienda shule, lakini wale walio katika madarasa ya juu bado wamefungiwa katika sehemu nyingi za nchi. Taliban iliahidi wasichana wote watarudi shuleni baada ya mwaka mpya wa Afghanistan mwishoni mwa Machi. Vyuo vikuu vinafunguliwa pole pole na vyuo vikuu binafsi na shule hazikuwahi kufungwa.
Umasikini unazidi kuongezeka. Hata wale ambao wana pesa wana wakati mgumu kuzipata. Katika benki, foleni ni ndefu na wakazi wanasubiri kwa saa nyingi, wakati mwingine hata siku nzima, ili kutoa kiasi kisichozidi $200 kwa wiki.
Zaidi ya dola bilioni 9 za mali za kigeni za Afghanistan zilizuiwa baada ya kundi la Taliban kuchukuwa madaraka. Wiki iliyopita, rais Joe Biden wa Marekani alitia saini mkataba alioahidi dola bilioni 3.5 kati ya dola bilioni 7 ya mali za Afghanistan zilizozuiwa nchini Marekani zitapewa familia za waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani. Dola bilioni 3.5 zilizosalia zitawekwa huru kwa ajili ya msaada wa Afghanistan.
Taliban imefanya kampeni ya kutambuliwa kimataifa utawala wake, lakini wanalazimishwa kuunda utawala unaojumuisha makundi yote na kuhakikisha unazingatia haki za wanawake na makundi ya walio wachache.
(ape)