Wanawake watatu wauwawa katika Maandamano ya Misri
20 Julai 2013Kulingana na taarifa kutoka idara ya afya nchini humo watu wengine saba wamajeruhiwa kwa visu na risasi za mpira jana katika maandamano.
Maandamano ya kumuunga mkono Rais Mursi yamekuja siku moja baada ya rais wa kipindi cha mpito nchini humo Adly Mansour akiapa kupigania udhabiti dhidi ya wapinzani aliowashutumu kwa kutaka kuipeleka Misri pabaya.
Maandamano pia yalifanyika katika maeneo mengine mjini Cairo na Alexandria baada ya chama cha udugu wa Kiislamu kuitisha maandamano yaliyopewa jina la " kuvunja mapinduzi ya kijeshi."
Mfuasi wa Mohammed Mursi aliezungumza na shirika la habari la AFP kwa njia ya simu amesema kwamba walikuwa wanaandamana katika mji huo wakati majambazi walipowavamia kwa risasi, visu na mawe.
Hali ya wasiwasi inaendelea kutanda nchini humo zaidi ya wiki mbili tangu jeshi lilipomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Hatua hii ilichukuliwa baada ya raia takriban milioni mbili nchini humo kuandamana dhidi ya utawala wa Mohammed Mursi.
Rais huyo hajaonekana hadharani hadi sasa huku viongozi wakuu katika chama chake cha udugu wa Kiislamu wakitiwa nguvuni.
" Naamini Mursi atarudi madarakani kwa uwezo wake maulana najua mwishowe nguvu ya wananchi itashinda," amesema mfuasi wa Mursi aliyetajwa kwa jina moja Mohammed mwenye umri wa miaka 45.
Mataifa ya nje yazungumzia hali ya Misri
Kwa upande wake msemaji wa mkuu wa masuala ya kibinaadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema mkuu wake alikuwa na mazungumzo na balozi wa Misri mjini Geneva na kuomba habari zaidi juu ya wale wote waliokamatwa na kufungamanishwa na matukio ya Julai 3 siku ambayo jeshi lilichukua madaraka na kumuondoa Mursi madarakani.
Katika masuala ya Kidiplomasia Uingereza ilisema kwamba inafuta leseni ya kusafirisha vifaa vinavyotumiwa na jeshi pamoja na polisi kwa kuwa na hofu kwamba huenda vifaa hivyo vikatumiwa dhidi ya waandamanaji.
Lakini kwa Upande wake Marekani hadi sasa imekataa kuiita hatua ya jeshi kama mapinduzi kwa kuwa inapokiri hilo basi moja kwa moja italazimika kukatiza msaada wao wa kijeshi wa dola bilioni 1.5 kwa jeshi la Misri.
Moja ya changamoto inayoikabili serikali ya mpito nchini Misri ni hali ya usalama hasa katika eneo la Sinai ambalo limekumbwa na ghasia wiki mbili zilizopita.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mhariri: Sekione Kitojo