Wanawake 2 wenye Corona wajifungua bila kuwaambukiza watoto
8 Aprili 2020Wanawake wawili wajawazito waliogundulika na virusi vya Corona nchini Peru wamejifungua watoto waliokutwa hawana maambukizi ya virusi hivyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na hospitali ya mji mkuu Lima Jumanne.
Mtoto wa kwanza alizaliwa tarehe 27 mwezi Machi na wa pili alizaliwa Machi 31 wote wawili walizaliwa kwa njia ya upasuaji kwa ushauri wa madaktari ili kuepusha matatizo mbali mbali. Daktari wa kitengo cha mausla ya familia katika hospitali ya Rebagliati Carlos Albrecht amesema kwa bahati nzuri hakuna maambukizi yaliyotokea na kwa maana hiyo watoto wote wamezaliwa vizuri na wako salama.
Pia wazazi wote wawili wameripotiwa kuwa katika hali nzuri ya kiafya ingawa bado wanapewa matibabu kutokana na kuwa na virusi vya Corona. Madaktari katika mji wa China wa Wuhan ambako ndiko mripuko wa virusi hivyo ulikoanzia walionesha wasiwasi mwanzoni mwa mwezi Februari kuhusu uwezekano wa kina mama wajawazito wenye virusi hivyo kuwaambukiza watoto wao watakaozaliwa baada ya kushuhudiwa kisa alau kimoja cha mtoto aliyezaliwa akiwa na dalili za ugonjwa wa COVID-19.
Shirika la afya duniani WHO limesema kwamba kina mama waliojifungua wenye maambukizi ya virusi vya Corona wanapaswa kutiwa moyo kuwatazama na kuwanyonyesha watoto wao kama kawaida almradi watatekeleza usafi wa kimsingi unaohitajika wakati wa kunyonyesha.
Kwa mujibu wa taarifa za madaktari, hili ni janga jipya na hakuna mwenye uzoefu nalo. China na Italia zimetowa machapisho kadhaa ambayo yanatowa maelezo kuhusu jinsi mama anavyoweza kumnyonyesha mwanawe mchanga. Lakini bado haijaelezwa kuhusu suala la maambukizi ya Mama kwenda kwa mtoto kupitia unyonyeshaji.
Imetajwa kwamba wanawake wenye dalili za kuwa na ugonjwa wa Covid-19 muongozi huenda ukatafautiana kwa maana hii watoto wachanga watalazimika kutenganishwa na mama zao. Hospitali ya Rebagliati mjini Lima imesema kupitia taarifa yake kwamba imefanya uchunguzi kwa mara nyingine kwa watoto hao wawili wachanga waliozaliwa na bado inasubiri majibu. Kufikia sasa Peru imethibitisha kuwa na visa 2,954 vya maambukizi ya virusi vya Corona na vifo 107 huku watu 1,301 wakitangazwa kupona.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Iddi Ssessanga