Wanawake Zimbabwe waanadamana
29 Oktoba 2008Wanawake hao walikusanyika nje ya Hoteli ya Rainbow Towers mjini Harare, mwanzoni huku wengi wao wakiwa wamevalia nguo za rangi nyeusi na nyeupe. Lengo lilikuwa ni kupinga mazungumzo ya muda mrefu sasa ya kugawana wizara muhimu baina ya vyama viwili vinavyohasimiana nchini Zimbabwe. Wakati wajumbe wa Chama cha Muungano wa Wanawake wa Zimbabwe(WCoZ) na Mradi wa Elimu ya Siasa cha Wanawake(FePEP) wakijaribu kuandaa maandamano hayo, polisi wa kutuliza ghasia waliwavamia ghafla na wanawake hao walitawanyika kuelekea katika maeneo tofauti. Baada ya hali kutulia, wanawake 47 walikuwa wamekamatwa, huku wengine 11 wakiwa wamejeruhiwa.
Wanawake hao walikuwa wakitafuta taarifa kuhusu kinachoendelea katika mazungumzo hayo. Walitaka kukutana na viongozi watatu waliosaini mkataba wa kugawana madaraka Septemba 15, mwaka huu, ambao ni Rais Robert Mugabe, Waziri Mkuu mteule Morgan Tsvangirai na naibu Waziri Mkuu mteule, Arthur Mutambara pamoja na timu ya usuluhishi.
Mwenyekiti wa Chama cha Muungano wa Wanawake wa Zimbabwe(WCoZ), Emilia Muchawa alisema mamia ya wanawake walikwenda mjini kwa ajili ya kufanya maandamano ya amani kwa sababu kama wake na akina mama, wanataka suluhu ya wakati mgumu wanaokabiliana nao.
Wanawake hao pia walikuwa wamedhamiria kuonyesha mateso wanayoyapata Wazimbabwe wa hali ya kawaida kwa wajumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, Mwenyekiti wa SADC Kgalema Motlanthe na ujumbe wake pamoja na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki na timu ya wapatanishi.
Polisi wamewafungulia mashitaka wanawake hao kwa kuingilia kifungu cha sheria ya jinai, kinachoeleza kuwa matukio yoyote ya kusababisha vurugu hadharani ni jinai. Sheria hiyo imekuwa ikitumika hivi karibuni kwa ajili ya kuvinyamazisha vyama vya kijamii nchini humo.
Hata hivyo Msemaji wa Polisi nchini Zimbabwe, Wayne Bvudzijena hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini afisa wa polisi mjini Harare, amesema polisi wana ushahidi kwamba kulikuwa na wahuni walioingilia maandamano ya wanawake hao na kutaka kuvuruga yasiendelee katika hoteli hiyo ya Rainbow Towers.
Musa Ndiraya, aliyekuwa akihudhuria mkutano wa washiriki wa zamani wa vita katika makao makuu ya ZANU-PF yaliyoko karibu na hoteli hiyo, amesema kulikuwa na wahuni wa chama cha Movement for Democratic Cahnge (MDC), waliojaribu kujifanya waonekane kama wanawake. Anasema walifanya hivyo pia wakati wa kutiliana saini makubaliano, mwezi uliopita. Watu hao hawataki kupatikana kwa suluhu ya mazungumzo hayo, kutokana na kukosekana kwa misaada kutoka kwa wahisani.
Wanawake hao waliachiliwa huru baadaye jioni ya siku waliyokamatwa baada ya wanasheria wa haki za binadamu kuingilia kati.
Huku wanawake hao wakikamatwa na kupigwa mjini Harare, jaji wa mji wa pili kwa ukubwa nchini Zimbabwe, Bulawayo, amekataa kuwapatia dhamana Jenni Williams na Magodonga Mahlangu, viongozi wa Chama cha Wanawake cha Zimbabwe (WOZA). Wanawake hao wawili walikamatwa Oktoba 16 kwa madai ya kuwaongoza wajumbe wa chama hicho kushiriki katika maandamano ya kuvipa changamoto vyama vya siasa nchini humo kumaliza haraka mazungumzo hayo ya muda mrefu.
Aidha, vitendo vya mshikamano kama hivyo vilikuwa vifanyike pia Johannesburg na Cape Town nchini Afrika Kusini, Oktoba 27, ambako mzozo huo wa Zimbabwe una madhara ya moja kwa moja.
Wakati wanawake wa WCoZ na FePEP pamoja na Wazimbabwe wengi wakiwa wamechoka kusubiri kufikiwa kwa mazungumzo hayo, vyama vitatu vimeshindwa kwa mara nyingine tena kugawana wizara nyeti ya Mambo ya Ndani. Mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya saa 15 chini ya SADC hayakufikiwa na hivyo kuahirishwa hadi katika mkutano mwingine wa SADC utakaofanyika baadaye.
Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kushindikana kwa mazungumzo hayo kunaweza kuathiri mpango mzima wa kugawana madaraka nchini Zimbabwe.