1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanazi na wapinzani wao wasababisha machafuko Chemnitz

Oumilkheir Hamidou
28 Agosti 2018

Mji wa Chemnitz, mashariki mwa Ujerumani uligubikwa na machafuko pale maelfu ya watu walipoteremka majiani kudai wageni waihame Ujerumani huku wapinzani wa siasa kali za mrengo wa kulia wakidai "wanazi" watoweke.

Deutschland Demonstration der rechten Szene in Chemnitz
Picha: picture-alliance/dpa/S. Willnow

Hali  ilianza kwa utulivu  jana usiku pale polisi walipoteremka kwa wingi kuzitenganisha pande hizo mbili zilizokuwa zikikodoleana macho na kukaripiana mbele ya sanamu kubwa la Karl Marx. Hali ilibadilika saa tatu za usiku pale waandamanaji walipoanza kutawanyika, watu kutoka makundi yote hayo mawili walipojeruhiwa kwa fataki na mawe yaliyokuwa yakivurumishwa na makundi ya watu waliovalia sare nyeusi , barkoa na miwani nyeusi.

Wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wakiripua fataki na kufanya fujo ChemnitzPicha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Maduka yalifungwa

Hali ilikuwa tayari inatisha hapo awali katika njia pana ya Brückenstrasse inayougawa mji wa Chemnitz ambako wapinzani wa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia waliitisha maandamano yao. Maduka, ambayo mengi yanamilikiwa na watu wenye asili ya Uturuki na kiarabu, yalifungwa mapema, pale makundi mawili, moja kutoka tawi la chama cha mrengo wa kushoto die Linke na la pili kutoka kundi la siasa kali za mrengo wa kulia-Pro Chemnitz walipoanza kidogo kidogo kukusanyika.

Nyimbo walizokuwa wakiimba si mpya katika eneo hilo la mashariki mwa Ujerumani: Miongoni mwao ni ile ya kumtaka kansela Merkel ang'atuke au mipaka ifungwe huku kundi la pili la waandamanaji wakipaza sauti kwa upande wao kudai "Wanazi watoweke na wakimbizi wanakaribishwe". Safari hii lakini maandamano yalichukua sura nyengine kabisa kutokana na kuuliwa katika sherehe za mji huo mjerumani mwenye asili ya Cuba aliyekuwa akijulikana sana na makundi yote ya kisiasa ya mji huo. Kijana huyo wa miaka 35 amefariki hospitali jumapili kutokana na majeraha aliyopata jumamosi usiku. Watu wawili wanaoripotiwa pia kuwa na asili ya wahamiaji, wamejeruhiwa katika shambulio hilo. Vijana wawili, muiraq wa miaka 22 na msyria wa miaka 23 wamekamatwa kutokana na mauwaji hayo.

Waziri wa sheria Katarina Barley ameonya dhidi ya mji wa Chemnitz kugeuka eneo lisilofuata sheria. Mwanasiasa huyo wa SPD amesema yeyote anaetishia usalama wa raia, anaewashambulia na kueneza chuki dhidi ya jamii ya wachache anabidi aandamwe kisheria. "Mitindo ya watu kuandamwa majiani na watu kujibebesha sheria mikononi mwao hairuhusiwi kabisa nchini Ujerumani.

Wafuasi wa makundi yanayopinga ubaguzi UjerumaniPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Maandamano zaidi yanatazamiwa kuitishwa siku zinazokuja

Kundi la wenye kupinga wageni-Pegida ambalo chimbuko lake ni jimbo hilo hilo la Sachsen linadai kijana huyo ameuliwa kwasababu ya kutaka kumlinda mkewe. Hawakutoa lakini ushahidi wowote wa hoja hizo. Machafuko ya Chemnitz yanatokea katika wakati ambapo maandhari ya kisiasa haijapambazuka kwa kansela Angela Merkel anaejikuta kila mara akikoselewa na wapinzani wake kwa kuwafungulia milango wageni.

Wimbi jengine la maandamano linapangwa kuitishwa katika miji mengine mnamo siku zinazokuja, ikiwa ni pamoja na Dresden.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/KNA

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW