Wanyamapori wasafirishwa kikatili kutoka Afrika
2 Septemba 2021Ripoti hiyo ya uchunguzi yenye kauli mbiu 'Cargo of Cruelty' inaonyesha namna mashirika ya ndege yanavyovuna pakubwa kutokana na biashara hii haramu, ikifichua kwamba zaidi ya aina 200 ya wanyamapori baadhi yao wakiwa wale walio kwenye hatari ya kutoweka, wamepatikana katika zaidi ya shehena 30 za mizigo iliyokuwa inasafirishwa na shirika la ndege la Fly Ethiopian kutoka Afrika kuelekea mataifa tofauti ulimwenguni.
Biashara hii sio halali katika mataifa mengi ya Afrika wanakopatikana wanyama hawa.
Akitoa mfano wa China na Congo, Jackson Kinyanjui, mtaalamu na msomi wa maswala ya mazingira anaonya kwamba hali ya wanyama pori kukaribiana sana na binadamu inasababisha msambao wa magonjwa sugu kama vile virusi vya corona na Ebola kutoka kwa wanyama kuingia kwa binadamu.
Aidha anasema wanyama hawa hukamatwa kwa njia ya kikatili na kusafirishwa katika mazingira duni.