1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapakistan wapiga kura licha ya mashambulizi na mauaji

25 Julai 2018

Licha ya ghasia, mashambulizi na mauaji kwenye vituo vya kupigia kura, upigaji kura umemalizika na vituo vimefungwa kwenye uchaguzi wenye ushindani mkali nchini Pakistani kati ya Imran Khan na Nawaz Sharif.

Pakistan Parlamentswahlen
Picha: Reuters/F. Aziz

Saa 12 jioni kwa majira ya Pakistan, vituo vilifungwa baada ya umma mkubwa kujitokeza vituoni kupiga kura zao wakikataa kutii vitisho vya makundi ya siasa kali ambayo yalifanya mashambulizi kwenye maeneo mbalimbali kabla na wakati wa upigaji kura wa leo.

Hadi kura ya mwisho inaingizwa kwenye kisanduku chake, ripoti zinaonesha kuwa watu 31 walishapoteza maisha kwenye jimbo la kusini magharibi la Baluchi, kutokana na mashambulizi ya kujitoa muhanga yaliyofanywa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS). 

Vyama vyote vikubwa kwenye uchaguzi huu, viliwatolea wananchi wito wa kutorudi nyuma kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Imran Khan, nyota wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa mkubwa wa upinzani, aliwaambia Wapakistan kuwa leo ilikuwa siku yao ya kubadilisha mfumo wa utawala wa taifa hilo pekee la Kiislamu lenye silaha za kinyuklia.

"Leo nawaambia Wapakistani wajitokeze kupiga kura. Wala sisemi kuwa mukipigie kura chama changu, pigia kura chama chochote, lakini ujuwe kuwa huu ni uchaguzi muhimu kwenye historia ya Pakistan. Hii ni mara ya kwanza tunapata nafasi ya kuvishinda vyama viwili ambavyo vimetutawala na kubadilishana utawala kwa zaidi ya miaka 30", alisema nyota huyo wa kriketi.

Awali Tume ya Uchaguzi ilikuwa imekataa maombi ya vyama kadhaa vya kisiasa ambavyo vilitaka muda wa kupiga kura uongezwe kwa saa moja zaidi.

Mpambano kati ya Khan na Sharif

Hakuna takwimu rasmi za waliojitokeza kupiga kura, lakini misururu mirefu ilionekana kwenye vituo tangu mapema asubuhi.

Nawaz Sharif, nyota wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa mkubwa wa upinzani nchini Pakistan.Picha: picture-alliance/AP Photo/K.M. Chaudary

Uchaguzi huu unaonekana kama mpambano mkali kati ya chama cha waziri mkuu aliyefungwa jela, Nawaz Sharif, na chama cha Khan.

Sharif aliyehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kutokana na makosa ya ufisadi, anakana tuhuma hizo akisema ni njama za wanajeshi na mahakama dhidi yake.

Aliwataka wapigakura kukipa chama chake, ambacho sasa kinaongozwa na kaka yake, muhula wa pili madarakani. Kwa upande wake, Khan amekuwa kiongozi wa muda mrefu sana wa upinzani, akijipambanuwa pia kama mpambanaji dhidi ya ufisadi.

Waandishi wa habari na wasimamizi wa uchaguzi wanasema kuwa mbali ya mashambulizi ya Quetta yaliyouwa watu 31, kwa ujumla sehemu nyengine za nchi zilipiga kura kwa amani.

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwenye uchaguzi huo, Michael Gahler, alilaani mauaji hayo ya Quetta, huku akisema walishindwa kwenda katika jimbo la Baluchistan kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara.

Mshindi rasmi anatarajiwa kujulikana saa nane za usiku majira ya Pakistan.

Uchunguzi wa kura za maoni kabla ya uchaguzi kufanyika ulikuwa unaoenesha kuwa hakutakuwa na chama kitakachopata wingi wa kutosha kuunda serikali peke yake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/dpa
Mhariri: Saumu Yussuf
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW