1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Baraza la Usalama lasogeza mbele kura juu ya vita vya Gaza

19 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesogeza mbele kura ya azimio la makubaliano mapya ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijadili mzozo wa Gaza | New York 2023
Picha ikionyesha sehemu ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baraza hili inatarajiwa kupiga kura Disemba 19, 2023 juu ya usitishwaji wa mapigano katika Ukanda wa Gaza Picha: YUKI IWAMURA/AFP

Kura hiyo iliahirishwa ili kuzuia kura nyingine ya Turufu ya Marekani wakati mazungumzo yakiendelea juu ya namna ya kuliandika azimio ambalo pengine Marekani, Israel na washirika wao wa karibuni watalikataa. 

Muswada huu wa karibuni zaidi umewasilishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu iliyoomba kura hiyo iliyopangwa kupigwa jana Jumatatu, majira ya saa 11 za jioni kusogezwa hadi asubuhi ya leo Jumanne, hii ikiwa ni kulingana na duru za kidiplomasia.

Muswada wa awali ulitoa mwito wa hatua endelevu na ya dharura ya kusimamisha machafuko katika Ukanda wa Gaza ili kuruhusu kupelekwa misaada ya kiutu.

Muswada huo huenda ukapunguzwa ukali wa maneno

Hata hivyo, ili kuzuia kura ya turufu ya Marekani, baadhi ya maneno katika muswada huo yanatakiwa kupunguzwa makali, wanasema wanadiplomasia ambao hawakutaka kutambulishwa walipozungumza na shirika la habari la AP. Muswada huo aidha unatoa wito wa kuachiwa huru mateka tena bila ya masharti yoyote pamoja na kulaani machafuko na mateso yote dhidi ya raia, lakini pia likipinga vikali visa vyote vya ugaidi.

Soma zaidi:Baraza la Usalama kukutana na waathirika wa vita vya Gaza

Mapema mwezi huu, Marekani ililipigia kura ya veto azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa likitoa wito wa kusitishwa mapigano ili kuruhusu upitishwaji wa misaada wa kiutu katika eneo hilo la Palestina lililoharibiwa vibaya na mashambulizi ya mabomu yanayoendelea kufanywa na Israel, ikijibu shambulizi la Hamas nchini mwake, mnamo Oktoba 7.

Mjini Washington, Wizara ya Mambo ya Nje imesema malori yaliyobeba misaada kuelekea Gaza, yakipitia Kivuko cha Kerem Shalom kilichofunguliwa siku ya Jumapili, yatasaidia kupunguza shinikizo lililopo kwenye Kivuko cha Rafah ingawa imesema bado misaada hiyo haitoshi.

Polisi wa Palestina akiwa amesimama pembeni mwa lori katika Kivuko cha Kerem Shalom katika Ukanda wa Gaza kinachotumika kupitisha misaada ya kiutu, septemba 5, 2023Picha: Khaled Omar/IMAGO

Msemaji wa wizara hiyo, Matthew Miller amesema "Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali za Israel, Misri na nchi washirika katika eneo hili ili kuongeza zaidi misaada ya kibinaadamu inayoingia Gaza ili kuwasaidia watu wa Palestina kupata mahitaji yao."

Amesema wanatumaini kuona ujia huo unaimarika na kupanuliwa katika siku zijazo, akisema ni hatua muhimu sana kuelekea kuboresha maisha ya Wapalestina kwenye eneo hilo. Ametoa taarifa hii siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin kujadiliana na viongozi wa Israel jana Jumatatu juu ya namna ya kupunguza mashambulizi huko Gaza, ingawa alisema Washington haipingani na mipango ya Israel, licha ya miito ya kimataifa ya kuitaka Israel kusitisha mapigano.

Israel yafanya mashambulizi mawili yaliyoua watoto na raia wa Palestina

Huku hayo yakiendelea huko Gaza kwenyewe, kuna taarifa kwamba karibu Wapalestina 10 wameuawa na wengine kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni watoto, baada ya Israel kufanya mashambulizi mawili katika jengo la makazi kusini mwa Gaza mapema leo. Majeruhi saba walikimbizwa katika hospitali ya Kuwait iliyoko Rafah na wengine walipelekwa katika hospitali ya al-Najjar.

Hadi sasa, zaidi ya Wapalestina 19,400 wameuawa hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, inayodhibitiwa na Hamas, wakati Umoja wa Mataifa ukikisia kwamba maelfu ya raia bado wamefukiwa na vifusi.

Soma zaidi: Israel yaendelea na mashambulizi Gaza

Katika hatua nyingine, Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Svenja Schulze anatembelea Israel na maeneo ya Palestina, kama sehemu ya ujumbe unaotafuta ukweli kufuatia vita hivyo. ofisi ya Svenja imesema, waziri huyo atakutana na jumuiya ya kiraia ya Israel na familia za waathirika wa shambulizi la Oktoba 7.

Atakutana pia na Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh, na kutembelea kambi ya wakimbgizi ya al-Amari iliyoko Ukingo wa Magharibi, akiambatana na wawakilishi wa Shirika la Kimataifa linalohudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA ili kuangazia mazingira ya kiafya na miundombinu ya elimu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW