1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina 43,508 wauawa Gaza

8 Novemba 2024

Idadi ya Wapalestina waliouawa kwenye Ukanda wa Gaza imefikia 43,508 tangu Israel ianze mashambulizi yake kwenye Ukanda huo miezi 13 iliyopita, huku jeshi la Israel likiviripua vijiji vitatu vya Lebanon kwa mabomu.

Gazastreifen | Zerstörung nach Luftangrif
Wapalestina wakisaka ndugu zao kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoshwa kwa mashambulizi ya Israel siku ya Jumapili (Novemba 4) kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: REUTERS

Wizara ya afya ya Gaza ilisema siku ya Ijumaa (Novemba 8) kwamba idadi hiyo ya wahanga wa vita vya Israel ilikuwa imeongezeka kufuatia vifo 39 vilivyotokea ndani ya masaa 24 yaliyopita, ikiongeza kuwa waliokwishajeruhiwa hadi hapo walishafikia 102, 684.

Israel ilianza awamu hii ya mashambulizi kwenye Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo wa Kipalestina kufanya uvamizi wa eneo la kusini la Israel mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, ambao ulipelekea vifo vya watu wapatao 1,200 na wengine 250 kuchukuliwa mateka. 

Soma zaidi: Mashambulizi ya Israel yawauwa watu 10 Gaza

Mapema Ijumaa, Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ilichapisha matokeo ya uchunguzi wake wa vifo vilivyotokea Gaza ndani ya miezi sita ya mwanzoni mwa mashambulizi hayo ya Israel, ambapo ilisema kuwa asilimia sabiini ya watu waliouawa walikuwa wanawake na watoto. 

Vijiji vyaporomoshwa kwa mabomu Lebanon

Katika upande mwengine wa mzozo wa Mashariki ya Kati, shirika rasmi la habari nchini Lebanon (NNA) liliripoti kwamba tangu asubuhi ya Ijumaa, jeshi la Israel lilikuwa likiendesha kampeni ya kuripua mabomu ndani ya vijiji vya Yaroun, Aitaroun na Maroun al-Ras katika eneo la Bint Jbeil, kwa lengo la kuyabomoa makaazi ya raia huko. 

Wanawake wa Lebanon wakabiliwa na kitisho cha uzazi salama

02:07

This browser does not support the video element.

Wanamgambo wa Hizbullah walisema walikuwa wakipambana na vikosi vya Israel kwenye eneo hilo, zaidi ya mwezi mmoja tangu Israel kuanza rasmi mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Lebanon, kufuatia kampeni ya Hizbullah kuirushia makombora kwa kile kundi hilo inachosema ni kuwaunga mkono ndugu zao wa Gaza.

Soma zaidi: Beirut yapigwa tena huku Israel ikitanua operesheni Gaza

Taarifa kutoka huko zilisema wanajeshi wa Israel walifanya pia msako kwneye mji wa karibu na Bint Jbeil, baada ya Hizbullah kusema ilivishambulia vikosi vilivyokuwa vikijaribu kuingia kijii cha Yaroun hapo jana.

Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran lilishambulia pia wanajeshi wengine wa Israel kwenye kijiji cha Maroun al-Ras.

Hali ya Gaza baada ya mashambulizi ya Israel.Picha: Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance

Miripuko ya mabomu iliyoshuhudiwa siku ya Ijumaa ilikuwa ya hivi karibuni ya aina hiyo kufanywa na jeshi la Israel katika vijiji vya mpakani mwa nchi hizo mbili. 

Kwa mujibu wa NNA, wanajeshi wa Israel waliyaporomowa majengo kwenye angalau vijiji saba vya mpakani mwezi uliopita.

Picha za video zilizothibitishwa na shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu (Novemba 5) zilionesha miripuko mikubwa kabisa ikisambaa kote kwenye kijiji cha Mais al-Jabal na kuzigeuza nyumba kuwa vifusi.

Mnamo mwezi Oktoba, kituo cha Channel 12 cha Israel, kilionesha video ya mmoja wa watangazaji wake akiliripuwa jengo moja wakati akiwa na wanajeshi wa nchi yake katika kijiji cha Aita al-Shaab.