Mladenov amepitiliza majukumu yake
12 Oktoba 2018Amesema mjumbe huyo ametafuta mkataba baina ya Israel na vuguvugu la Kiislamu la Hamas.
Ahmed Majdalani ambaye ni mwanachama wa kamati ya utendaji ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO amesema wamemfahamisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba Nikolay Mladenov hakubaliki tena na serikali ya Palestina.
Mladenov hajazungumza kuhusu suala hilo
Majdalani amesema Mladenov amekwenda hatua zaidi kupita jukumu lake katika kutafuta makubaliano kati ya Israel na kundi la Hamas ambalo linadhibiti eneo la Gaza na kudai kwamba vitendo vyake vinahujumu usalama wa kitaifa wa Palestina na umoja wa watu wake.
Hakujakuwa na kauli kutoka kwa Mladenov kuhusiana na suala hilo wala thibitisho kutoka kwa Umoja wa Mataifa. Mladenov kwa ushirikiano na Misri amekuwa akitafuta makubaliano ya amani ya muda mrefu baina ya Hamas na taifa hilo la Kiyahudi, bila kuijumuisha katika mazungumzo hayoserikali ya Rais wa palestina Mahmud Abbas inayotambulika kimataifa.
Mazungumzo hayo yamekwama kwasababu ya shinikizo kutoka kwa Abbas lakini Jumanne iliyopita makubaliano madogo yaliyoongozwa na Umoja wa Mataifa yalifikiwa ambapo Qatar ilitakiwa kufadhili usafirishwaji wa mafuta yanayohitajika sana Gaza kwa kipindi cha miezi sita.
Uongozi wa Palestina ulipoteza udhibiti wa Gaza 2007
Serikali ya Rais Abbas haikushirikishwa katika makubaliano hayo na mpango wa Mladenov umewaghadbisha wanasiasa wa Palestina.
Uongozi wa Palestina unaoongozwa na Mahmoud Abbas una uhuru wa kiasi katika sehemu kadhaa za Ukingo wa Magharibi lakini ikapoteza udhibiti wa Gaza kwa kundi la Hamas mwaka 2007 katika vita vilivyokaribia kuwa vya wenyewe kwa wenyewe.
Tokea wakati huo Jamii ya Kimataifa imefanya kazi na Uongozi wa Palestina. Chama cha Ukombozi wa Palestina kimeitambua Israel na kimetia saini mikataba kadhaa ya amani nayo huku ikiwa Hamas imepigana vita vitatu na taifa hilo la Kiyahudi tangu mwaka 2008.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman