Wapalestina kuteua makamu wa rais kumsaidia Abbas aliyezeeka
24 Aprili 2025
Katika muktadha wa vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas, uongozi wa Palestina unaonekana kuchukua hatua za ndani za kurekebisha muundo wake wa kisiasa.
Rais Mahmoud Abbas, mwenye umri wa miaka 89 na anayekumbwa na ukosoaji mkubwa, ameanza kushinikiza mageuzi ambayo huenda yakamuandalia nafasi mrithi wake wa moja kwa moja kwa mara ya kwanza.
Taarifa kutoka Ramallah zinasema kuwa Baraza Kuu la Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) linajadili kubuni nafasi mpya ya makamu wa rais, ambayo itaambatana na wadhifa wa naibu mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya PLO.
Hii ni hatua ambayo inaweza kufungua njia ya wazi kwa mpangilio wa urithi wa Abbas — jambo ambalo limekuwa likihitajika kwa muda mrefu.
Ingawa haijulikani kama nafasi hiyo itajazwa mara moja, kiongozi anayependekezwa zaidi ni Hussein al-Sheikh, mshirika wa karibu wa Abbas na katibu mkuu wa PLO tangu 2022.
Al-Sheikh ameongoza mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mamlaka ya Palestina na Israel kwa miaka kadhaa, na ana ushawishi mkubwa ndani ya mfumo wa sasa.
Uundwaji wa nafasi ya makamu unakuja wakati mamlaka ya Palestina inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wafadhili wa mataifa ya Magharibi na Kiarabu kufanya mageuzi, ili iweze kuwa sehemu ya usimamizi wa Gaza baada ya vita.
Soma pia: Hamas, Fatah kufanya mazungumzo ya maridhiano China
Hata hivyo, Israel haijaonesha nia ya kuruhusu mamlaka hiyo kushiriki katika utawala wa eneo hilo, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akisisitiza kuwa Israel itaendelea kudhibiti usalama wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Matamshi makali dhidi ya Hamas
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa kamati kuu ya PLO siku ya Jumatano, Abbas alitumia lugha kali dhidi ya Hamas, akiwaita "wana wa mbwa” - jambo lililowashangaza wengi na kukosolewa na baadhi ya wanasiasa wa Palestina kama Mustapha Barghouti, aliyesema kuwa lugha hiyo "inazidisha migawanyiko."
Abbas pia aliitaka Hamas kuwaachilia mateka waliobaki na kuweka chini silaha, akidai kuwa hilo lingepunguza visingizio vya Israel vya kuendeleza mashambulizi.
Wakati huo huo, orodha ya watu wanaoweza kumrithi Abbas inaendelea kupanuka. Mbali na Hussein al-Sheikh, kuna Majed Faraj, mkuu wa usalama wa Palestina, Jibril Rajoub ambaye ameonekana kujipatia umaarufu kupitia soka, na Mohammed Dahlan ambaye anaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Soma pia:Ushindi wa Netanyahu wawaudhi Wapalestina
Hata hivyo, jina linalotajwa sana katika kura za maoni ni Marwan Barghouti, kiongozi wa Fatah aliyefungwa maisha na Israel kwa makosa yanayohusiana na mashambulizi wakati wa Intifada ya pili.
Hata kama nafasi ya makamu wa rais itaundwa, bado kuna ukungu mkubwa juu ya lini Abbas ataondoka madarakani, au iwapo ataachia kwa hiari.
Kilicho wazi ni kwamba hatima ya kisiasa ya Palestina iko katika kipindi cha mpito kigumu, ambapo maslahi ya ndani na nje yanakutana, huku swali kuu likibaki: Je, mrithi wa Abbas ataweza kuyaunganisha maeneo hayo na kuleta mwelekeo mpya?
Chanzo: Mashirika