1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waadhimisha miaka 77 tangu tukio la Nakba

15 Mei 2025

Wakati vita vikiendelea kusababisha maafa makubwa huko Gaza huku Israel ikidhihirisha mpango wake wa kulitwaa eneo hilo, vitendo hivyo vimewakumbusha Wapalestina tukio la "Nakba", ambalo huadhimishwa Mei 15 kila mwaka.

Nakba ya mwaka 1948: Wapalestine wakilazimika kuondoka kwenye makazi yao
Nakba ya mwaka 1948: Wapalestine wakilazimika kuondoka kwenye makazi yaoPicha: PicturesFromHistory/CPA Media/IMAGO

Neno Nakba au al-Nakba ambalo kwa lugha ya kiarabu linamaanisha janga au maafa, linamaanisha tukio la Wapalestina kupoteza ardhi yao kati ya miaka ya 1947 na 1949, kabla  Israel  kutangaza rasmi kuwa taifa mnamo Mei 14, 1948 baada ya vita kati ya mataifa ya kiarabu na Israel, ili kupinga mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuigawanya Palestina.

Inadhaniwa kuwa takriban watu 700,000 katika eneo ambalo sasa ni taifa la Israel ama walikimbia au walilazimishwa kuyahama makazi yao, jambo lililopelekea wakimbizi wengi wa Kipalestina kuishi wakiwa hawana utaifa hadi leo hii.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, tangu wakati huo, Wapalestina wengi wamekuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi ambazo baada ya muda ziligeuka kuwa miji katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na  Jerusalem Mashariki,  Lebanon, Syria, Jordan huku idadi ndogo ya Wapalestina wengine wakiondoka kabisa eneo hilo na kuomba uraia wa nchi zingine.

Wapalestina wakiishi kwenye mahema nchini Jordan baada ya Nakba ya mwaka 1948Picha: PicturesFromHistory/CPA Media/IMAGO

Mzee huyu wa Kipalestina bi Badryeh Mohareb anakumbuka madhila waliyopitia wakati wa Nakba ikiwa miaka 77 iliyopita:

" Vita vyote vilivyoshuhudiwa eneo hili, hakuna vita vinavyoweza kulinganishwa na Nakba. Vita hivyo vilikuwa vya kikatili mno. Nyumba yangu ilibomolewa na hawakuniachia chochote. Niliondoka nyumbani kwangu mikono mitupu, nilikuwa na nguo tu nilizovaa, bila blanketi, wala godoro, sikuwa na chochote, Naapa kwa Mungu."

 Vita vya Gaza vyaendelea kurindima

Idadi ya vifo kufuatia mashambulizi ya Israel leo Alhamisi imefikia watu 94 huku wengine watano wakiuliwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Mamlaka za Gaza zimesema watu wengine 60 wameuawa kufuatia mashambulizi mapya ya Israel huko  Gaza.

Jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya Israel huko Khan Younis, Ukanda wa GazaPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi mtendaji wa  Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch HRW Federico Borello amesema vizuizi vinavyosababishwa na mzingiro wa Israel huko Gaza sasa vimekuwa zaidi ya mbinu ya kijeshi na vimegeuka 'chombo cha maangamizi' kwa Wapalestina.

Wakati huhuo  kundi la Hamas  limekosoa kile walichokiita kuwa "uamuzi wa makusudi" wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wa kuidhinisha wimbi jipya la mashambulizi huko Gaza likisema kuwa hatua hiyo inahujumu juhudi za upatanishi ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka, mazungumzo ambayo yameonekana kukwama.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW