1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waendelea kukwama umoja wa mataifa

Sekione Kitojo31 Desemba 2011

Miezi mitatu baada ya makaribisho ya mbwembwe aliyoyapata rais wa Palestina Mahmoud Abbas katika umoja wa mataifa ,hakuna dalili za hatua kupigwa kufikia kutambuliwa.

Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akiwa katika baraza kuu la umoja wa mataifa.
Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akiwa katika baraza kuu la umoja wa mataifa.Picha: AP

Wakati rais wa mamlaka ya ndani wa Palestina Mahmoud Abbas alipohutubia mataifa 193 wanachama wa Umoja wa mataifa katika mkutano mkuu mwezi Septemba,makaribisho ya mbwembwe aliyoyapokea yaliashiria uungwaji mkono katika harakati za kutaka taifa hilo kutambuliwa na umoja huo,lakini miezi mitatu baadaye,hakuna dalili zozote za hatua kupigwa katika kulifikia hilo la kutambuliwa na kukubaliwa kuwa mwanachama kamili wa Umoja huo wa mataifa na baraza la usalama la umoja huo kwasababu wapalestina wamenyamaa kimya pengine kutokana na shinikizo kutoka kwa Marekani.

Samir Sanbar ambaye alikuwa msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja huo na anayefahamu kwa undani siasa za mashariki ya kati aliliambia shirika la habari la IPS kuwa utawala wa Palestina haujafanya lolote kutafuta kuungwa mkono na mataifa wanachama wa baraza la usalama,kabla na baada ya hotuba ya Rais Abbas kwa umoja huo iliopokelewa vyema.

Sanbar ameongeza kuwa tangu Palestina ilivyoitenga Umoja wa mataifa kama mpatanishi mkuu katika mchakato wa kutafuta amani katika mazungumzo na Israeli na kutafuta usaidizi kwingineko tangu mwaka 1992,utawala wa Palestina haujaonekana kurejea kikamilifu katika Umoja huo.

Sanbar ambaye amehudumu chini ya makatibu watano tofauti wa Umoja huo ikiwemo kuwa mkuu wa idara ya mawasiliano kwa umma,anasema raia wa Palestina ambao ni waathiriwa wa mzozo huo, wanaendelea kutaabika. Kwa sasa mataifa 125 yanaitambua Palestina kama taifa huru nje ya kanuni za Umoja wa mataifa.

Mwezi Septemba,Rais Abbas aliwasilisha rasmi ombi kwa katibu mkuu wa Umoja huo Ban Ki Moon la kutaka Palestina itambuliwe na kuwa mwanachama kamili licha ya pingamizi kali kutoka kwa Marekani.

Kamati ya baraza la usalama la Umoja huo lililo na wanachama 15 imegawanyika vikali bila ya kufikia mapatano kuhusu uanachama wa Palestina.

Marekani inatarajiwa kutumia kura yake ya turufu kupinga jaribio lolote la kuleta ombi hilo la Palestina mbele ya baraza hilo.

Palestina hata hivyo ina njia mbadala ya kutambuliwa na Umoja huo, kwa kuwasilisha ombi la kupewa hadhi maalum kama Vatican

Rais wa baraza kuu la Umoja huo Balozi Nasir Abdelaaziz al Nasser wa kutoka Qatar, wiki iliyopita aliwaambia waandishi wa habari kuwa amesikia Abbas anajaribu kupanga mikakati ya serikali yake na kutatua masuala kadhaa ya Palestina kabla ya kuliwasilisha ombi hilo mbele ya mkutano huo mkuu.

Kikao cha baraza kuu la umoja wa mataifa kikiendeleaPicha: dapd

Rais huyo amesema kuwa Palestina inahitaji tu wingi mdogo wa kura kupandishwa katika hadhi na uwezekano wa kufanikiwa kwa hilo ni mkubwa.

Mwandishi: Caro Robi/IPS

Mhariri: Sekione Kitojo.