Wapalestina waishi katika hali ngumu Ukanda wa Gaza
12 Desemba 2025
Mvua kubwa zilizoandamana na upepo mkali zilisababisha mafuriko ambayo yamezidi kutatiza hali ya maisha na raia wa Palestina wanaoishi katika kambi mbalimbali. Familia kadhaa zimekabiliwa na hali ambapo vyakula vyao, malazi na vitu vingine vimelowa majini kufuatia mvua hizo katika mazingira magumu wanaoishi kwenye mahema na magofu ya majengo yaliyoharibiwa katika vita.
Um Salman Abu Qenas, mwanamke ambaye familia yake ipo katika kambi ya mahema ya Khan Younis, amesimulia jinsi walivyoshindwa kulala baada ya magodoro yao kulowa maji huku wakikumbwa na baridi kali inayotishia kuwasababishia magonjwa.
Taka zilizorundikana bila kuondoshwa kwenye makazi hayo ya muda zimekuwa vyanzo vya harufu mbaya na pia kutishia kuchafua maji yanayotumiwa na binaadamu. Lakini jeshi la Israel linalaumiwa kwa hali hiyo kwa kutotimiza ahadi ya kuruhusu angalau lori 600 za shehena za misaada ya kibinadamu kila siku kuwafikia wahanga hao.
Hii imefanya watu kuishi katika msongamano kwenye mahema ambayo hayawezi kukidhi idadi yao pamoja na uhaba wa vitu muhimu vya kimaisha.
UNRWA yasema hali inayoshuhudiwa iliweza kuepukika
Shirika la Umoja Mataifa la misaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA limetaja madhila yanayowakumba watu hao kuwa yangeepukika kama wangepata vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuwezesha mazingira safi ya makaazi, dawa pamoja na mahema ya kutosha.
Shirika hilo limetaja kupokea taarifa kutoka kwa watu zaidi ya 2,500 wakitaka misaada ya dharura kufuatia mafuriko hayo. Itakumbukwa kuwa zaidi ya watu milioni mbili wa Palestina walilazimika kuyahama makaazi yao katika vita hivyo na wengi wanaishi katika kambi za muda. Mama mwingine kwa jina Amina Abdalla amesimulia hali inayowakumba kwa kusema:
"Usiku tunazama na magodoro yetu. Tunahitaji kwa dharura malazi na hata nguo zetu zimelowa. Watoto wangu wanajaribu kuchimba mitaro kwa shida ili kuachilia maji yaende. Huku majirani nao wakiwa wanatusaidia hatujui kama tutalala leo mimi mama mjane na watoto wangu yatima. Pengine majirani watatusaidia."
Hata sehemu za Kusini mwa kati mwa Israel zimekumbwa na mafuriko hayo na kuwasababisha watu kadhaa kukwama katika magari yao. Shirika la Jeshi la Israel linalowashughulikia uwasilishaji wa misaada COGAT limesisitiza kuwa katika mwezi huu wa Desemba limewesha mahema 260,000 kufikishwa kwa kambi za Wapalestina ziliwasilishwa na malori 1,500. Lakini Baraza la Wakizimbi la Norway linadai kuwa idadi hiyo inayotajwa si ya kweli.
Kwingineko shirika la Amnesty International kwa mara ya kwanza limetoa ripoti inayoshutumu kundi la Hamas kwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu kwa raia wa Israel tangu kuzuka kwa vita mwezi Oktoba mwaka 2023.
Katika ripoti yake ya kurasa 173, shirika hilo linasema kuwa Hamas walifanya mashambulizi ya kimakusudi katika maeneo ya kiraia na kusababisha vifo vya watu 1,200 huku wakiwachukua mateka 2,500 waliowatendea ukatili mbalimbali ikiwemo manyanyaso ya kingono.
Kwa upande wake, Israel inadaiwa kuwaua zaidi ya wapalestina 70,000 zadi ya nusu yao wakiwa wanawake na watoto. Msemaji wa Wizara ya mambo ya kigeni wa Israel Oren Marmorstein ameunga mkono ripoti hiyo lakini akahoji kwa nini imechukua zaidi ya miaka miwili kwa Amnesty kuitoa.
Kupitia ukurasa wake wa X ametaja idadi hiyo hata kuwa ndogo kuliko hali ilivyokuwa.