1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wanaendelea kuteseka

Kabogo Grace Patricia14 Mei 2010

Matamshi hayo yametolewa na mpatanishi wa ngazi ya juu wa Palestina, Saeb Erakat.

Moja ya mitaa ya mji wa Jerusalam Mashariki.Picha: AP

Mpatanishi wa ngazi ya juu wa majadiliano kutoka upande wa Palestina, Saeb Erakat amesema Wapalestina wanaendelea kukumbana na maafa miaka 62 baada ya kuundwa kwa taifa la Israel, hatua iliyosababisha maelfu ya wakimbizi. Bwana Erakat ametoa matamshi hayo ikiwa kama ujumbe wake wa siku ya maafa inayojulikana kama Naqba, ambayo kumbukumbu yake inafanyika kesho Jumamosi.

Saed Erakat amesema kuwa maafa yanaendelea na kusisitiza kuwa wakimbizi ambao kwa pamoja na vizazi vyao sasa wamefikia milioni 4.7, wana haki ya kurejea nyumbani. Katika migogoro mingine, haki za wakimbizi zinaheshimiwa na kuthaminiwa, ikiwemo haki ya kurejea na malipo ya fidia.

Hata hivyo, Israel imekataa hata kutambua suala la haki ya kurejea kwa wakimbizi hao, hivyo kuendelea kukazikataa haki za msingi za wakimbizi. Erakat amesema kuwa hakuna taifa ambalo liko juu ya sheria, na kuitolea mwito jumuiya ya kimataifa kuitaka Israel iache kuzipuuzia sheria za kimataifa. Mpatanishi huyo wa Palestina amesisitiza kuwa ni lazima lianzishwe taifa huru la Palestina, huku eneo la Jerusalem Mashariki likiwa kama mji wake mkuu.

Siku hiyo ya maafa-Naqba, ni maalum kwa ajili ya kukumbuka maafa ya Wapalestina yaliyotokana na kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948, ambapo Waarabu 700,000 waliyakimbia na wengine kufukuzwa katika makaazi yao. Katika kuadhimisha siku hiyo, usiku wa leo mishumaa itawashwa katika kambi za wakimbizi huku maandamano makubwa yakipangwa kufanyika Palestina hapo kesho, ikiwemo kuzuru kaburi la kiongozi wa zamani wa Mamlaka ya Palestina, Yasser Arafat huko Ramallah, mji mkuu wa kisiasa unaokaliwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi.

Wakati huo huo, msemaji wa polisi nchini Israel, amesema kuwa uchanguzi kuhusu mauaji ya kijana wa Kipalestina anayesemekena ameuawa na walowezi wa Kiyahudi, umeanza. Mwili wa kijana huyo Aysar Zaben, mwenye umri wa miaka 16, ulipatikana katika Ukingo wa Magharibi hii leo, ingawa inadaiwa kwamba aliuawa jana. Kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi, haijafahamika wazi nini hasa kilitokea au nani anahusika na tukio hilo.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa kundi la vijana wa Kipalestina walirusha mawe katika gari lililowabeba walowezi wa Kiyahudi walipokuwa wakipita katika barabara karibu na mji wa Ramallah. Baada ya kutupiwa mawe, walowezi hao wenye silaha waliwafyatulia risasi vijana hao waliokuwa wakirusha mawe. Kifo hicho ni cha kwanza kutokea kati ya pande hizo mbili tangu Israel na Palestina zianze mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja Jumamosi iliyopita. Kiasi walowezi wa Kiyahudi 500,000 na kiasi Wapalestina milioni 2.5 wanaishi katika Ukingo wa Magharibi na maeneo karibu na eneo la Jerusalem lililochukuliwa kwa nguvu na Israel baada ya kushinda vita vya Mashariki ya Kati, mwaka 1967.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW