1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Scholz atoa wito wa mshikamano na Wayahudi

8 Desemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameviita vitisho dhidi ya jamii ya Kiyahudi kuwa ni vya kusikitisha na kutisha, huku akitoa wito wa mshikamano na jamii ya Wayahudi nchini Ujerumani.

Siku ya kuwasha mishumaa - Berlin
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akihutubia umma wakati wa tukio la kuwasha mshumaa kuashiria maadhimisho ya sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah kwenye Lango la Brandenburg huko Berlin, Desemba 7, 2023.Picha: Tobias Schwarz/AFP

Kansela Scholz ametoa wito huo wakati jamii hiyo ikianza maadhimisho ya sikukuu ya Hanukkah. Hannukah, hubeba dhima ya matumaini na ujasiri, mambo ambayo kulingana na Scholz yanahitajika sana katika nyakati za sasa. Kansela Scholz alikuwa kwenye tukio la kuwasha mshumaa mjini Berlin, kuashiria kuanza kwa sikukuu hiyo.

Amesema, shambulizi la kigaidi la Hamas nchini Israel liliwashtusha sana na kuongeza kuwa kila mtu anatakiwa kuupinga ugaidi kwa uwazi.

Soma pia: Scholz aahidi kuwalinda Wayahudi dhidi ya vitendo vya chuki

Ujerumani imeshuhudia kuongezeka kwa visa vya uhalifu dhidi ya Wayahudi, ambapo tangu Oktoba 7 hadi Novemba 9, imerekodi visa 994 vya chuki dhidi ya jamii hiyo. Idadi hii inamaanisha kwa siku kulishuhudiwa visa 29, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia 320 ikilinganishwa na vile vilivyorikodiwa kila siku, mwaka uliopita, hii ikiwa ni kulingana na Taasisi inayosimamia Idara za Utafiti na Taarifa juu ya Chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.

Jeshi la Israel lawazuia waandamanaji wanaotaka udhibiti zaidi wa Wayahudi huko Jerusalem

Huko Israel, jana jioni, jeshi la nchi hiyo limezuia maandamano ya wafuasi wa siasa za mrengo mkali wa kulia katika mji mkongwe wa Jerusalem.

Maafisa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji wa mrengo mkali wa kulia waliokuwa wakielekea Mji Mkongwe wa JerusalemPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Soma pia: Mapigano makali yaendelea Ukanda wa Gaza 

Waandamanaji walikuwa wakishinikiza kurejeshwa kwa udhibiti kamili wa Wayahudi kwenye mji wa Jerusalem ikijumuisha eneo takatifu kwa wayahudi, waislamu na wakristo ambalo limekuwa kitovu cha mvutano kwenye mji huo wa kale. Waandamanaji hao walinuia kukatiza kwenye viunga vya msikiti wa Al-Aqsa eneo ambalo ni la tatu kwa utukufu miongoni mwa waumini wa dini ya kiislamu na kisha wavuke kuingia Mji Mkongwe kabla ya kuelekea kwenye mabaki ya ukuta wa hekalu takatifu la Wayahudi.

Vyombo vya habari vya Israel vimearifu kwamba polisi waliwazuia waandamanaji, kwa kuwa baadhi yao walikiuka masharti ya makubaliano na jeshi hilo ya kutobeba mabango ama kuimba nyimbo zenye ujumbe wa uchochezi.

Soma pia: Israel yashambulia mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.:

Mapema, Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu- OIC ililaani hatua ya Israel ya kuruhusu maandamano hayo, iliyoyaita ni ya uchokozi.

Mtu akiwa anatembea katikati ya vifusi vya jengo lililoharibiwa na shambulizi la bomu la Israel usiku kucha huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza mnamo Desemba 7, 2023.Picha: MAHMUD HAMS/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine, mtaalamu wa masuala ya ugaidi, Justin Crump, ambaye pia ni mkuu wa taasisi ya ushauri wa masuala ya usalama ya nchini Uingereza ya Sibylline, amesema mapigano yanayoendelea sasa kusini mwa Gaza yamekuwa yakichukuliwa kama mapigano makali kabisa katika vita hivyo hadi sasa, na Israel imekuwa ikitumia mbinu zilezile ilizozitumia ilipokuwa inapambana na  Hamas, kaskazini mwa Gaza.

Crump ameiambia DW kwamba, mkakati huo pia unafanana na uliotumiwa na Marekani na Uingereza wakati zilipoivamia Iraq mnamo mwaka 2003, kwa kuingia kwenye maeneo ya miji kutoka pande tofauti tofauti, kulizingira eneo na kuendesha msako kwenye maeneo ambayo Israel inayachukulia kuwa hatari na yanayolengwa zaidi.

Amesema lengo la Israel la kuliangamiza kundi la Hamas, halina mantiki kijeshi, hata kama jeshi lake litafanikiwa pakubwa vitani, kwa kuwa mafanikio hayo kamwe hayataweza kuifuta fikra ya Hamas. Ameongeza kuwa operesheni ya kijeshi pekee haitaweza kuleta suluhu ya tatizo lililopo, akiangazia Gaza na hali ya usalama nchini Israel.

Kulingana na Umoja wa Mataifa raia wengi hivi sasa wanaukimbia mji wa Khan Younis kutokana na mapigano makali yanayoendelea kwenye mji huo, na kuelekea Rafah, kusini mwa Gaza. Umoja huo umesema watu milioni 1.87 ambao ni sawa na asilimai 80 ya idadi ya watu kwenye Ukanda wa Gaza wamekimbia makazi yao tangu kuanza kwa vita hivyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW