1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina warejea Khan Younis baada ya Israel kuondoka

8 Aprili 2024

Israel iliviondoa vikosi vyake kusini mwa Ukanda wa Gaza na mji mkuu wa eneo hilo Khan Younis, hatua iliyowaruhusu Wapalestina wengi waliopoteza makaazi kurejea katika eneo hilo lililoharibiwa vibaya kwa mabomu.

Khan Yunis
Wakaazi wa Khan Yunis warudi katika mji huo ulioharibiwa vibaya kwa mashambulizi kati ya Israel na HamasPicha: AFP/Getty Images

Israel imeongeza shinikizo, ikionya kuwa iko tayari kuanzisha operesheni kamili za kijeshi dhidi ya Hamas katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, eneo la mwisho ambalo mpaka sasa halijavamiwa na vikosi vya ardhini.

Soma pia: Israel yakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu vita vyake Gaza

Israel iliviondoa vikosi vyake kusini mwa Ukanda wa Gaza na mji mkuu wa eneo hilo Khan Younis, hatua iliyowaruhusu Wapalestina wengi waliopoteza makaazi kurejea katika eneo hilo lililoharibiwa vibaya kwa mabomu.

Lakini Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant alisisitiza kuwa lengo lilikuwa ni kwa vikosi vya Israel "kujiandaa kwa operesheni za usoni, ikiwemo mjini Rafah," kwenye mpaka na Misri. "Mafanikio ya vikosi vilivyofanya kazi huko Khan Yunis ni makubwa sana. Kuwapiga magaidi, kuyaharibu maeneo ya adui, maghala, silaha, mahandaki, makao makuu, vyumba vya mawasiliano, mambo haya yote yalitekelezwa kwa njia ya kuridhisha sana, na hivyo Hamas ikashindwa kufanya kazi ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza."

Mazungumzo ya kusitishwa mapigano na kuwachiwa mateka wanaoshikiliwa Gaza yanaendelea CairoPicha: Presidency of Egypt/Anadolu/picture alliance

Wakati hayo yakiendelea, juhudi za amani zinaendelea Cairo. Shirika la Habari lenye uhusiano wa karibu serikali ya Misri, Al-Qahera limeripoti kuwa "hatua kubwa imepigwa kuhusu vipengele kadhaa vyenye utata, likitaja chanzo kimoja cha ngazi ya juu cha Misri.

Limesema wajumbe wa Qatar na Hamas waliondoka Cairo na wanatarajiwa kurejea katika siku chache zijazo ili kukamilisha masharti ya makubaliano. Wajumbe wa Marekani na Israel pia walitarajiwa kuondoka kwa ajili ya kufanya mashauriano.

Afisa mmoja wa Hamas ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa kuhusu Gaza na hakuna chochote kipya katika mazungumzo ya Cairo.

Malori ya misaada yaliingia Gaza jana kupitia kivuko cha Rafah, nazo bidhaa za matibabu zikaingizwa kupitia kivuko cha Erez cha Israel katika upande wa kaskazini.

Wakati vita vikiendelea Gaza, mashariki ya kati imeshuhudia machafuko yanayoyahusisha makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran nchini Lebanon, Syria, Iraq na Yemen.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

02:51

This browser does not support the video element.

Jeshi la Israel – IDF limesema leo limemuuwa kamanda mwandamizi wa Kikosi cha Radwan cha Hezbollah. IDF imesema Ali Ahmed Hassin na wapiganaji wengine wawili waliuawa katika mji wa kusini mwa Lebanon wa Sultaniyah. Hezbollah imethitibisha kifo cha kamanda huyo lakini haikutoa maelezo zaidi.

Mjini The Hague, Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ imeanza leo kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Nicaragua, inayotaka Ujerumani kuacha kuipatia Israel msaada wa kijeshi na misaada mingine, kwa kuzingatia madai kwamba Berlin inasaidia vitendo vya mauaji ya kimbari na kukiuka sheria ya kimataifa ya kiutu katika vita kati ya Israel na Hamas.

Nicaragua iliyowasilisha kesi hiyo inadai kwamba hatua ya Ujerumani kuipatia Israel msaada wa kisiasa, kifedha na kijeshi na kuondoa ufadhili kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina, UNRWA inaashiria wazi kwamba wanaratibu mauaji ya kimbari na kwa namna yoyote ile wameshindwa kutimiza wajibu wa kufanya kila linalowezekana kuzuia mauaji ya kimbari.

afp, dpa, ap, reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW