Wapalestina watatu wauwawa Ukingo wa Magharibi
12 Machi 2023Wanajeshi wa Israel wamewauwa kwa kuwapiga risasi wapiganaji watatu wa Kipalestina katika mapigano ya kabla ya alfajiri ya leo katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa duru kutoka pande zote mbili yaani Israel na Palestina, katika kipindi hiki ambacho kumeendelea kuripotiwa ongezeko la ghasia katika eneo hilo.
Kundi la wapiganaji lenye maskani yake mjini Neblus lilisema vikosi vya Israel vilifanya uvamizi katika eneo lao.
Wizara ya Afya ya Palestina imewatambulisha waliouawa kuwa Jihad al-Shami, mwenye umri wa miaka 24, Uday al-Shami, miaka 22, na Mohammad Dabeek miaka 18.
Ghasia ziliongezeka mwaka jana, lakini zimezidi kuwa mbaya katika eneo la Ukingo wa Magharibi, ambao Israel imeukalia kimabavu tangu Vita vya Siku Sita vya 1967.
Kurejea madarakani kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mwezi Disemba akiwa mkuu wa muungano wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia kumeongeza mtafaruku.