1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Muda wa kusitisha mapigano Gaza watarajiwa kurefushwa

29 Novemba 2023

Kundi la sita la mateka wa Israel linatarajiwa kuachiwa huru leo huku wapatanishi wa kimataifa wakijaribu kutafuta kurefushwa kwa muda zaidi wa kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas

Ukanda Gaza| Utafutaji wa wahanga wa mashambulizi ya Israel.
Wapalestina wametumia kipidi cha usitishaji mapigano kutafuta watu waliokwama kwenye vifusi vya mashambulizi ya Israel.Picha: Ismail Muhammad/UPI Photo via Newscom picture alliance

Wapatanishi wanaotafuta kuongezwa kwa muda wa kusitishwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas, huko Gaza wanaamini kuwa muda huo unaweza kuongezwa kwa siku mbili zaidi. Haya ni kulingana na vyanzo viwili vya usalama vya Misri. Vyanzo hivyo vimearifu kuwa idadi ya mateka wa kiraia wanaoshikiliwa na Hamas ambao wanapaswa kuachiwa huru chini ya makubaliano hayo bado inafanyiwa kazi. Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kadhaa ya Magharibi yameliorodhesha kundi la Hamas kuwa la kigaidi. Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa yakiendelea vizuri, lakini mateka wa kijeshi wanaoshikiliwa na Hamas walileta vikwazo.

Mtoto mmoja na kijana wauawa kwa risasi zilizofyatuliwa kutoka upande wa jeshi la Israel

Wizara ya afya ya Palestina imesema kuwa Adam al-Ghul, mwenye umri wa miaka minane, na Bassem Abu el-Wafa, mwenye umri wa miaka 15, waliuawa kwa risasi zilizofyatuliwa kutoka upande wa jeshi la Israel. Picha za CCTV zinazosambaa mtandaoni na kwenye habari za televisheni zinaonesha mvulana akipigwa risasi na kuanguka barabarani, na kusababisha watoto wengine kukimbia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa - Antonio GuterresPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Soma pia: Usitishaji vita waibua matumaini ya mateka zaidi kuachiwa

Picha nyingine zinaonyesha kijana mmoja pia akipigwa risasi na kuanguka, kisha akionekana kuomba msaada huku risasi nyingi zikipiga chini karibu naye wakati watu wengine wakikimbilia usalama wao. Hata hivyo jeshi la Israel bado halijatoa taarifa kuhusu matukio hayo.

Umoja wa Mataifa waitaka jumuiya ya kimataifa kuangazia suluhu la mataifa mawili

Umoja wa Mataifa leo umeitaka jumuiya ya kimataifa kuangazia suluhu la mataifa mawili kwa mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas, ikisema kwamba Jerusalem inapaswa kutumika kama mji mkuu wa mataifa yote mawili ya Israel na Palestina.

Wakati alipokuwa akisoma taarifa ya katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres, mkurugenzi mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Tatiana Valovaya, amesema wakati umewadia wa kuchukuwa hatua thabiti na zisizopaswa kubatilishwa katika kuafikia suluhu la mataifa mawili kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Valovaya ameongeza kuwa hii itamaanisha Israel na Palestina zinaishi pamoja kwa amani na usalama huku Jerusalem ikiwa mji mkuu wa mataifa yote mawili.

Soma pia:Israel-Gaza zatakiwa kuongeza muda wa kusimamisha mapigano

Msichana aliyetekwa nyara na kundi la Hamas akumbatiana na babake baada ya kuachiwa huruPicha: Israel Defense Forces/REUTERS

Maoni hayo yanalingana na siku ya Mshikamano wa Umoja wa Mataifa na Watu wa Palestina, ambayo inaadhimishwa kila mwaka. Siku hii ni kumbukumbu ya kuidhinishwa kwa mpango wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wa kugawanya kwa Palestina kuwa mataifa ya Kiarabu na Kiyahudi na utawala wa kimataifa juu ya Jerusalemu.

Wanaharakati wa Utruki kupeleka msaada katika ukanda wa Gaza

Katika hatua nyingine, wanaharakati wa Uturuki wanataka kupeleka msafara wa meli zilizobeba msaada katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa, hii ikiwa sehemu ya kampeni ya kimataifa. Haya ni kulingana na mwakilishi wa shirika moja katika eneo hilo Behesti Ismail Songür aliyeliarifu shirika la habari la dpa hii leo.

Soma pia:Marekani yatuma ndege za misaada ya kibinadamu Gaza

Songür, ameliarifu shirika la dpa kwa njia ya simu kwamba lengo lao ni sawa na la Mavi Marmara. Songür alikuwa anazungumzia tukio la mwaka 2010 wakati makomando wa Israel walipoivamia meli ya Mavi Marmara na kuwaua wanaharakati 10. Meli hiyo ilikuwa inajaribu kuvuka kizuizi cha kuelekea Gaza na kusababisha mvutano wa kidiplomasia. Songhur anasema wanafanya mazoezi ya uasi wa kiraia na kwamba wanataka Israel kuondoa vizuizi vyake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW