Italia yakataa mageuzi ya Meloni katika kura ya maoni
24 Machi 2026
Huku karibu kura zote zikiwa zimehesabiwa, matokeo ya kura ya maoni ya kikatiba iliyopigwa Jumapili yanaonesha upande wa "Hapana" unaopinga mageuzi hayo una asilimia 53.5, na wa "Ndiyo" ukiwa na asilimia 46.5. Karibu asilimia 59 ya wapiga kura walijitokeza ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Waziri Mkuu Meloni hata hivyo amesisitiza kuwa haendi kokote. Amesema Wataliano wamezungumza na kwamba uamuzi wao utaheshimiwa, akiongeza kuwa hilo halitabadilisha dhamira yao ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa na kuheshimu jukumu walilopewa na umma.
Wakati wa kampeni za kura ya maoni, alisema mara kwa mara kwamba kura hiyo -- ambayo ilihusu jukumu na usimamizi wa majaji na waendesha mashtaka -- haikuhusu uongozi wake mwenyewe. Lakini alifanya kampeni kali ya kuyapigia debe mapendekezo hayo, pamoja na washirika wake wa muungano katika serikali ya mrengo wa kulia, huku vyama vya upinzani vikipigania kura ya "Hapana".