1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura wahitimisha uchaguzi wa bunge la Ulaya

9 Juni 2024

Wapiga kura kote Ulaya wanapiga kura zao Jumapili katika siku ya mwisho na kubwa zaidi ya uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya huku vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vikitarajiwa kupata mafanikio makubwa.

Ubelgiji | Wapiga kura katika kituo cha kura mjini Brussels
Wapiga kura katika kituo cha kura mjini BrusselsPicha: Kenzo TRIBOUILLARD/AFP

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa katika nchi 21 wanachama, zikiwemo Ufaransa na Ujerumani, kwa ajili ya uchaguzi huo ambao utatoa muelekeo wa Umoja wa Ulaya kwa miaka mitano ijayo.

"Uchaguzi huu ni muhimu kwa sababu bunge la Ulaya lazima lianze kutekeleza jukumu lake halisi," Kostas Karagiannis amealimbia shirika la habari la AFP baada ya kupiga kura yake mjini Athens.

Uchaguzi huu unajiri wakati bara la Ulaya linakabiliwa na vita vya Urusi nchini Ukraine, mivutano ya kimataifa ya kibiashara na kiviwanda inayotokana na ushindani wa Marekani na China, athari za mabadiliko ya tabianchi na nchi za Magharibi ambazo katika miezi michache ijayo huenda itabidi zizoee utawala mpya wa Donald Trump.

Soma pia: Wapiga kura barani Ulaya washiriki uchaguzi wa bunge la Ulaya

Zaidi ya watu milioni 360 wanastahili kupiga kura kote katika mataifa 27 wanachama wa Umoja wa UIaya. Uchaguzi huo ulianza Alhamisi wiki hii, ijapokuwa ni kundi dogo tu linalotarajiwa kupiga kura zao.

Matokeo yatatoa sura ya muundo wa Bunge lijalo la Umoja wa Ulaya ambalo husaidia katika kuamua nani anayeongoza Halmashauri Kuu ya Ulaya, ambapo kiongozi wa kihafidhina wa Ujerumani Ursula von der Leyen anagombea kwa muhula wa pili.

Matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa leo jioni.

Usalama ni moja ya vipaumbele vya wapiga kura

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akipiga kura yake katika kituo cha kura eneo la Burgdorf karibu na Hanover, Ujerumani.Picha: Fabian Immer/REUTERS

Wapiga kura wengi wanaozongwa na gharama kubwa ya maisha na hofu kwamba wahamiaji huenda wakawa chanzo cha upotofu wa maadili, wanazidi kushawishiwa na wanasiasa wanaoegemea siasa za mrengo mkali wa kulia.

Mpiga kura raia wa Hungary Ferenc Hamori mwenye umri wa miaka 54, amesema anataka kuuona Umoja wa Ulaya ukiongozwa na wanasiasa wenye sifa kama alizonazo Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban.

Na katika nchi zilizo karibu na Urusi, kitisho cha moja kwa moja kutoka Moscow kinachukuliwa kama dira ya kuamua wampigie nani kura.

"Suala la usalama ni kipaumbele changu,” amesema daktari Andrzej Zmiejewski mwenye umri wa miaka 51, baada ya kupiga kura katika mji mkuu wa Poland, Warsaw.

Soma pia: Uchaguzi wa Bunge la Ulaya kudhoofisha muungano wa Scholz? 

Ufaransa inatajwa kuwa uwanja wa mapambano wa fikra zinazokinzana.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Marine Le Pen kinatabiriwa kukishinda kile cha kiliberali chake Rais Emmanuel Macron.

Katika mji wa Ufaransa wa Lyon, Albert Coalaudon mwenye umri wa miaka 83, amesema Macron ameanza "kuchanganyikiwa” kutokana na kujihusisha na masuala mengi kama vile vita vya nchini Ukraine.

Coalaudon ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hali hiyo inamtisha.

Umaarufu wa chama cha AfD waongezeka Ujerumani

Mfuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia akibeba bendera ya AfD na UjerumaniPicha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance

Nchini Ujerumani, taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, uchaguzi huo wa bunge la Ulaya unaweza kuwa pigo kwa Kansela Olaf Scholz, ambaye chama chake siasa za wastani za mrengo wa kushoto SPD kiko nyuma ya kile cha Mbadala wa Ujerumani AfD.

Chama kinachoongoza kuelekea uchaguzi huo ni chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Christian Democratic Union - CDU kikiwa na uungwaji mkono wa asilimia 30, nacho chama cha AfD kikiwa na uungwaji mkono wa asilimia 14 mbele ya vyama vitatu katika muungano tawala: SPD, chama cha kijani na kile cha kiliberali cha FDP.

Matokeo mabaya ya chama cha SPD yatatafsiriwa kama nuksi kwa Olaf Scholz miezi mitatu tu kabla ya kufanyika uchaguzi katika majimbo matatu mashariki mwa Ujerumani, ambapo chama cha mrengo mkali wa kulia AfD kinatabiriwa kufanya vizuri.

Uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 pia unakaribia na nafasi ya Olaf Scholz kuendelea kusalia kama Kansela inaonekana kuwa ndogo.

Soma pia: Nani kuchukua usukani wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya

Muungano tawala wa Scholz unahitaji kujipanga upya japo uchaguzi wa bunge la Ulaya unaofanyika Jumapili nchini Ujerumani – hautarajiwi kwa namna yoyote ile kukiongezea umaarufu chama chake cha SPD na muungano tawala.

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Lothar Probst mwenye makao yake mjini Bremen, Kansela Scholz hachukuliwi kama mwanasiasa mwenye sauti imara ndani ya Ulaya kuelekea uchaguzi huo wa bunge la Ulaya.

Probst ameliambia gazeti la Handelsblatt kuwa, "kwa matokeo ya kawaida tu ya chama chake, Scholz anakabiliwa na hatari ya kupoteza imani ya wapiga kura na hata uungwaji mkono ndani ya chama chake.”

Kama hiyo haitoshi, idadi kubwa ya Wajerumani wanaonekana kutoridhika na uongozi wa Scholz huku asilimia 59 wakieleza kutoridishwa naye, kwa mujibu wa utafiti wa kura ya maoni hivi karibuni.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi