Wapiga kura wengi waunga mkono Uhuru wa Kurdistan
26 Septemba 2017Tume ya uchaguzi imesema idadi ya waliyoshiriki kura ya maoni hapo jana ilikuwa zaidi ya asilimia 72. Matokeo rasmi ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa kutolewa ndani ya siku tatu. Baada ya kupiga kura wakurdi walisherehekea usiku mzima mjini Erbil, mji mkuu wa Iraq katika eneo la Kurdistan.
Mamilioni wa wakurdi walishiriki kura hiyo licha ya onyo kutoka kwa jamii ya kimataifa na majirani zake. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema imesikitishwa na hatua ya serikali ya jimbo la Kurdistan kuandaa kura hiyo ya maoni.
"Mahusiano ya kihistoria kati ya Marekani na watu wa Kurdistan hayatabadilika kufuatia kura hiyo lakini tunaamini hatua hii itasababisha kutokuwepo na uthabiti na kuzidisha maisha magumu katika eneo la Kurdistan na watu wake." Ilisema Wizara hiyo ya Marekani katika taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumapili.
Maafisa wa kikurdi nchini Iraq walianza kuhesabu kura katika jimbo la Kurdistan na maeneo mengine yaliyokuwa na utata kuanzia saa moja usiku.
Kulingana na tume ya uchaguzi watu milioni 5.6 walisajiliwa na kuwa na haki ya kupiga kura katika vituo 2,065 katika jimbo hilo la Kurdistan na maeneo mengine yanyodhibitiwa na wakurdi Kaskazini mwa Iraq.
Kura hii imefanyika licha ya kupingwa vikali na serikali ya Iraq inayoitaja kuwa kinyume na katiba ya nchi.
Serikali ya Iraq yakosolewa kwa kutounga mkono kura ya maoni ya wakurdi
Huku hayo yakiarifiwa Waziri mkuu wa wakurdi nchini Iraq Nechirvan Barzani ameikosoa serikali ya Iraqi na mataifa jirani wanaoipinga kura ya maoni iliyofanyika jana na inayotaka Uhuru wa jimbo la Kurdistan.
Amesema serikali yake inatarajia kufanya mazungumzo ya kina na majirani zake wa kikanda kuhakikisha kunakuwepo na mahusiano mazuri kwa maslahi ya pamoja na heshima. Ameongeza kuwa watu wake wanatumia haki yao kuamua mustakbal wao, huku akisema wamechukizwa na misimamo ya mataifa mengi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Awali Naibu rais wa Iraq Nuri al-Maliki alisema kura hiyo ni kutangaza vita dhidi ya umoja wa watu wa Iraq. Umoja wa Mataifa pia ulionya kwamba kura hiyo huenda ikayumbisha usalama. Nao majirani wa Iraq: Uturuki, Iran na Syria wameingiwa na wasiwasi kwamba huenda wakurdi katika maeneo yao wakataka kujitenga. Kufuatia wasiwasi huo Uturuki imesema huenda ikaliwekea vikwazo jimbo la Kurdistan na kuwataka raia wake kutoitembelea mikoa iliyoandaa kura hiyo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Iran Bahram Ghassemi amesema nchi yake imefunga mipaka yake na Kaskazini mwa Iraq baada ya ombi la kufanya hivyo kutolewa na Waziri wa mambo ya nje wa Iraq.
Hata hivyo Israel imekuwa nchi pekee iliyounga mkono kura ya maoni ya Kurdistan ya Uhuru wa jimbo lao na kujitawala wenyewe. Mapema mwezi huu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Israel inaunga mkono juhudi halali za wakurdi kupata taifa lao.
Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga