1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapigakura 3000 huenda wasishiriki uchaguzi Uganda

Saleh Mwanamilongo
22 Desemba 2020

Shirika la haki za binadamu la Human Rigths Watch limeitaka tume ya uchaguzi nchini Uganda kuwahakikishia maelfu ya wanavijiji kaskazini mwa nchi hiyo haki yao ya kupiga kura.

Global Ideas | Uganda | Recycling-Projekte
Picha: DW/J. Mugambwa

Kwenye taarifa yake, shirika la Human Rights Watch limesema kwamba wapigakura wapatao elfu tatu na mia tano, huenda wasishiriki kwenye uchaguzi mkuu wa Januari 14 mwakani. Raia hao wote ni wakaazi wa kijiji cha Apaa, kaskazini mwa Uganda.

Kufuatia zoezi la kurekebisha daftari ya wapigakura, tume ya uchaguzi haikuwaorodhesha wapiga kura kutoka kijiji hicho, sababu ni kwamba serikali ilitangaza kwamba kijiji cha Apaa ni eneo la mbuga ya hifadhi ya wanyama ya East-Madi. Na kwa zaidi ya miaka kumi sasa, vikosi vya usalama vimekuwa vikiwaandama raia hao. Otsieno Namwaya ni mtafiti mwandamizi kwenye shirika la Human Rigts Watch kuhusu Uganda:

Shirika la Human Rights Watch limesema mwaka 2018, wakaazi 243 wa kijiji cha Apaa, walilazimika kutembea zaidi ya kilomita 100 ili kuomba hifadhi kwenye shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Gulu, baada ya jeshi kuchoma makaazi yao. Walirejea makwao baada ya siku 30, wakati spika wa bunge na maafisa wa balozi za Danemark, Norway na Umoja wa Ulaya kuwahakikishia kupata suhulisho la mzozo huo.

Mwezi Agosti mwaka 2018 , Rais Yoweri Museveni aliunda tume iliyoongozwa na waziri mkuu wa Uganda kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mzozo huo wa Apaa, lakini hadi sasa hakuna suluhisho lililopatikana.

Rais Yoweri Museveni na Bobi Wine

Februari mwaka huu, Spika wa bunge la Uganda aliiomba serikali kusitisha hatua yake ya kuwafukuza na kuwahamisha wakaazi wa Apaa, lakini serkali iliendelea na operesheni yake ya kuwalazimisha raia hao kuyahama makaazi yao.Vituo vitatu vya kupigia kura viliondolewa na tume ya uchaguzi kwenye kijiji hicho. Viongozi walifunga soko la Apaa na kuwalazimisha wakaazi wake kuhamia kwenye kijiji cha Zoka, umbali wa kilomita 40.

Baadhi ya wapigakura wameliambia shirika la HRW kwamba tume ya uchaguzi iliweka majina yao kwenye vituo vingine vya kupigia kura. Hali ambayo itawalazimisha kutembea kilomita kadhaa kwa mguu ili kupiga kura. Ferdinand Oreja, mwenye umri wa miaka 31, mmoja wa waliohojiwa na shirika la HRW amesema kwamba jina lake limeorodheshwa kwenye kituo kilichoko umbali wa kilomita 50 kutoka kijiji cha Apaa. Mwanzoni mwa mwezi Desemba, Shirika la HRW liliiandikia tume ya uchaguzi kuhusu madai hayo lakini hadi sasa tume hiyo haijatoa jibu lolote.

Ofisi ya takwimu ya Uganda inaelezea kwamba kijiji cha Apaa kina wakazi 11,000 lakini ukaguzi usio rasmi uliofanywa nyumba hadi nyumba na jamii ya Apaa inaelezea kwamba kijiji hicho kina wakaazi 26,000.
 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW