1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viktor Orbán wa Hungary ashindwa uchaguzi

13 Aprili 2026

Wapiga kura nchini Hungary wamemwondoa madarakani Waziri Mkuu wa muda mrefu Viktor Orbán na kuhitimisha enzi ya sera kali za kizalendo kutoka kwa mwanasiasa huyo aliyechagua usuhuba na Urusi.

Uchaguzi wa Bunge, Hungary 2026 | Raia wa Hungary akisherehekea mjini Budapest matokeo ya uchaguzi
Raia wa Hungary akisherehekea mjini Budapest matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumapili.Picha: Denes Erdos/AP Photo/picture alliance

Katika kile kinachozingatiwa kuwa ujumbe usio na mashaka kutoka kwa wapiga kura wa Hungary, Viktor Orbán amebwagwa vibaya sana kwenye uchaguzi wa jana Jumapili na kuhitimisha miaka 16 ya utawala wake uliogemea siasa za kizalendo na ukuruba na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa Viktor Orbán aliye pia ni rafiki kipenzi wa Rais Donald Trump wa Marekani ambaye hivi majuzi tu alimtuma makamu wake JD Vance kwenda Hungary kumpigia kampeni mwanasiasa huyo.

Ziara hiyo ya JD Vance wala halikufua dafu, na inaonesha wapiga kura wa Hungary walikwishafikia uamuzi wa kuzikataa sera za kiimla za Orbán na ajenda yake ya kuongoza vuguvugu la kihafidhina ambalo kwa miaka kadhaa iliyopita limetishia kuitenga Hungary ndani ya Umoja wa Ulaya.

Wananchi wa Hungary badala yake wamempa kazi ya Uwaziri Mkuu, Peter Magyar, aliyepata wakati fulani kuwa mtu wa karibu sana wa Orban lakini katika uchaguzi wa mwaka huu akaamua kujitenga naye. Aliendesha kampeni kubwa dhidi ya rushwa na kuboresha masuala ya kila siku yanayowagusa raia kama afya na usafiri wa umma.

Bunge jipya litakapoundwa, Chama cha Magyar cha Tisza kinatazamiwa kutapata viti visivyopungua 138 katika bunge lenye vita 199 la Hungary.

Magyar asema umma wa Hungary "umerejesha nchi mikononi mwao"

Peter Magyar akishangilia ushindi baada ya matokeo ya uchaguzi nchini Hungary. Picha: Denes Erdos/AP Photo/picture alliance

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliojitokeza kushangilia ushindi nje ya viunga vya majengo ya bunge mjini Budapest, Péter alisema, "Hatukushinda kidogo, tumeshinda, tena sana. Kwa pamoja tumeubadili utawala wa Orban, pamoja tumeikomba Hungary, tumerejesha nchi mikononi mwetu"

Kuangushwa kwa Orban na chama chake cha Fidesz kunatazamiwa kuleta ahueni ndani ya Umoja wa Ulaya hasa kutokana na misimamo yake ya kupinga sera za umoja huo na ukaribu wake na Urusi.

Viongozi wa Ulaya watakuwa na matumaini kwamba ushindi wa Magyar unafungua njia ya kuufanyia mageuzi mfumo wa kisiasa wa Hungary ambao kwa miaka kadhaa sasa Brussels imekuwa ukisema "unatishia desturi za kidemokrasia."

Katika mahojiano aloyafanya hivi karibuni kabla uchaguzi, Magyar aliahidi kurekebisha mahusiano yake na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo alijizuia kutoa msimamo wa wazi kuhusu masuala tata kama sera kali dhidi ya ushoga zilizowekwa na serikali ya Orbán na iwapo Hungary itaongeza uungaji wake mkono kwa Ukraine.

Viongozi wa Ulaya wampongeza kwa wingi kiongozi ajaye wa Hungary 

Waziri Mkuu aliyepoteza uchaguzi nchini Hungary, Viktor Orbán:Picha: Bernadett Szabo/REUTERS

Viongozi wa mataifa ya Ulaya hawajaficha hisia zao kwenye kushangilia ushindi wa mpinzani wa Orbán.

"Hivi leo Ulaya imeshinda na maadili ya Ulaya yameshinda," ndivyo alivyosema Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Katika salamu zake za pongezi Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani ameandika kuhusu haja ya kuunganisha nguvu pamoja kwa Ulaya iliyo na mshikamano.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi yake inaukaribisha kwa mikono miwili ushindi huo wa kidemokrasia wa watu wa Hungary.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Keir Starmer wa Uingereza ameutaja ushindi wa Magyar kuwa wa kihistoria, "siyo kwa Hungary pekee bali kwa demokrasia ya Ulaya".

Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya  amesema, "Hungary imechagua Ulaya na Ulaya imeichagua Hungary".

Salamu za pongezi zimetoka pia kwa viongozo wa Denmark, Romania, Slovenia, Ireland, Sweden na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW