1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji 300 wa Burundi waingia DRC na kuzusha hofu

Mitima Delachance22 Oktoba 2018

Kunaripotiwa mapambano makali kati ya jeshi la Congo, FARDC na waasi katika eneo la Ruzizi, Kivu kusini.

Demorkatische Republik Kongo - Soldaten der Democratic Republic of Congo nach Kämpfen mit Rebellen
Picha: Reuters/G. Tomsaevic

Wakaazi wa bonde la Ruzizi  katika  Kivu kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaishi katika hofu baada ya wapiganaji zaidi ya 300 kutoka Burundi kuvuka mpaka wa Congo hadi katika milima upande huo. Kunaripotiwa mapambano makali kati ya jeshi la Congo, FARDC na waasi vijiji kadhaa vya eneo hilo.

Mapambano hayo kati ya jeshi la Congo na waasi hao wa FNL yameripotiwa tokea usiku wa kuamkia leo  jumatatu  eneo la Katogota kandokando na kilalo kwenye mto Luvumvi unaopakana na Kamanyola, baada ya wapiganaji hao warundi kujipenyeza katika kijiji hicho tangu saa tatu usiku.

Wakazi wa Sange pia wanasema kwamba milio ya risasi imesikika tangu Jumamosi na jumapili baada ya wapiganaji hao toka Burundi kuvuka bonde la Ruzizi hadi katika ya milima ya Kabunambo na Rukobero ndani ya ardhi ya Congo. 

Kambi ndogondogo za wapiganaji wa Burundi zipo Uvira-DRC?

Kuna madai ya mara kwa mara ya kuwepo kambi za wapiganaji wa Burundi nchini DRc

Mara kwa mara kumekuwa kukiripotiwa uwepo wa kambi ndogo-ndogo za wapiganaji kutoka Burundi katika milima ya wilaya ya Uvira, na jeshi la Congo FARDC kuwarudisha nyuma. Naibu msemaji wa jeshi katika kivu kusini kapteni Dieudonné Kasereka amesema kwamba kundi hilo ni watu wanaotaka tu kufanya uporaji ndani ya bonde la Ruzizi.

Mjini Bukavu, wakaaji wanahisi kwamba ikiwa hali hii itaendelea, huenda ikachangia katika kuzorotesha usalama wa uchaguzi unaopangwa kufanyika hivi karibuni.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, waziri wa mambo ya ndani na usalama hapa kivu kusini, Victor Chomachoma amependekeza kwamba serikali za Congo na Burundi zikutane na kuchukua hatua muhimu haraka iwezekanavyo kuhusu tabia hii ya kujipenyeza kwa wapiganaji hao wa FNL katika ardhi ya Congo.

Hadi sasa, inaripotiwa bado mapiganao makali yanaendelea katika milima ya Munanira, Lubarika na Muhungu ambamo wapiganaji hao wanafuatiliwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na makundi ya wanamgambo wa kujitolea wakiwemo wapiganaji wa Mai-Mai.

 

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW