1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji 31 wa Boko Haram wajisalimisha Niger

Oumilkheir Hamidou
28 Desemba 2016

Zaidi ya wanamgambo 30 wa Boko Haram wamesalim amri katika jimbo la Diffa, kusini mashariki ya Niger, hatua inayodhihirisha kudhoofika kundi hilo la wanamgambo wa itikadi kali wanaoitikisa Nigeria na nchi jirani.

Niger Soldaten in Bosso
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

"Vijana 31 wa Diffa walioingizwa miaka iliyopita katika kundi la wanamgambo wa Boko Haram, wamesalim amri" amesema waziri wa mambo ya ndani wa Niger kupitia mitandao ya kijamii, alipokuwa ziarani Diffa, mji unaopakana na eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria-ngome ya Boko Haram.

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa Niger kuzungumzia juu ya kutoroka raia wao toka makundi ya Boko Haram wanaofanya mashambulio ya kikatili tangu mwaka 2015 nchini Niger pia.

"Wamesalim amri, mmoja baada ya mmoja na wamewekwa hivi sasa katika kituo salama" duru za usalama kutoka Diffa zimesema. Wanawake watatu ni miongoni mwa wanamgambo hao 31 waliosalim amri. Mwanamke mwengine wa nne ambae ni raia wa Nigeria, nae pia ametoroka na kusalim amri mbele ya maafisa wa serikali katika jimbo la Diffa.

 

Wakimbizi wanasaidiwa kuingia ndani ya magari kurejea nyumbani NigerPicha: picture-alliance/dpa/EPA/Stringer

Vijana wanategemea msamaha wa serikali

"Tumetoroka toka kundi la Boko Haram kwasababu tumegundua kwamba visa vinavyofanywa na kundi hili havikubaliki.Tunataraji serikali itatusaheme na kutusaidia tusifikirie tena kujiunga na kundi kama lile" amesema hayo mpiganaji mmoja wa zamani kupitia kituo cha televisheni ya taifa.

Vijana hao wanaweza kusamehewa na kabla ya kurejea katika familia zao watajiunga na mradi wa mafunzo ya jinsi ya kujiambatanisha na maisha ya kijamii na kiuchumi nchini"-duru za usalama zimesema.

January mwaka jana, afisa mmoja wa serikali ya jimbo la Diffa alizungumzia juu ya kuondoka "vijana kadhaa" na kujiunga na Boko Haram waliokuwa wakiwaahidi vijana hao kuwalipa hadi faranga laki tatu-kiwango ambacho ni sawa na Euro 500 kwa mwezi."Baadhi walikuwa wakirejea na pesa ili kuzisaidia familia zao, jambo lililokuwa likiwavutia vijana wengine wengi.Tangu wiki kadhaa zilizopita hali inasemekana ni utulivu katika eneo la kusini mashariki mwa Niger ambako hujuma za Boko Haram zimepungua sana..

Vikosi vya usalama, polisi na raia wamekusanyika mahala shambulio la kuyatoa mhanga maisha lilikotokea MaiduguriPicha: Getty Images/AFP/STR

Watu wanarejea majumbani mwao pia nchini Nigeria

Niger Chad na Nigeria zimeanzisha  kwa wakati mmoja mwezi July mwaka huu opereshini ya kuwavunja nguvu Boko Haram katika ngome zao. October iliyopita serikali ya Niger ilisema opereshini hizo zimeanza kuleta tija na maeneo kadhaa yamekombolewa.

Wakati huo huo zaidi ya wakaazi 3000 wa kaskazini mashariki mwa Nigeria, waliolazimika kuyahama maskani yao kutokana na hujuma za Boko Haram, wamefanikiwa kurejea nyumbani baada ya njia muhimu zinazoiunganisha Maiduguri mji mkuu wa jimbo la Borno na miji ya Damasak na Baga kufunguliwa upya.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/Mhariri

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW