1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Wapiganaji tisa wanaoiunga mkono serikali Yemen wauawa

16 Agosti 2024

Wapiganaji tisa wanaoiunga mkono serikali nchini Yemen wameuawa katika shambulio la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika kambi ya kijeshi kusini mwa nchi hiyo.

Jemen | Luftangriff auf Ibb 2015
Picha: dpa/picture-alliance

Msemaji wa baraza la mpito la kusini mwa Yemen TSC Mohammed al-Naqib ameeleza kuwa, gari lililobeba vilipuzi lilishambulia kambi hiyo ya kijeshi mkoa wa Abyan.

Al-Naqib ameliambia shirika la habari la AFP kuwa shambulio hilo limewajeruhi pia wapiganaji wengine 13 na kwamba idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka.

Afisa mwengine wa jeshi amethibitisha shambulio hilo japo ameeleza kuwa idadi ya waliouawa ni kumi na moja, tofauti na iliyotolewa na Al-Naqib.

Afisa huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu hajapewa idhini ya kuzungumza na waandishi wa habari, pia amelilaumu kundi la Al-Qaeda kwa kuhusika na hujuma hiyo.

Yemen ni kitovu cha makundi ya kigaidi kama vile Al-Qaeda tawi la rasi ya kiarabu AQAP, linalochukuliwa na Marekani kuwa mojawapo ya makundi hatari ya itikadi kali za dini ya Kiislamu.