1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wa al-Shabaab wavuruga amani Mogadishu.

24 Agosti 2010

Wabunge 10 wa Somalia wameuliwa kwa kuchinjwa walipovamiwa hotelini na wapiganaji wa al-Shabaab.

Watu 97 wamejeruhiwa katika vita mjini Mogadishu.Picha: AP

Wapiganaji wa kundi la al-Shabaab nchini Somalia wanaendelea kuvuruga amani katika mji mkuu Mogadishu ambapo tayari kiasi ya watu 29 wameuawa katika mashambulio yao. Habari za hivi punde zinasema kwamba wapiganaji hao wameivamia hoteli moja karibu na ikulu ya rais na kuwauwa watu 42 wakiwemo wabunge 10.

Afisa wa polisi mjini Mogadishu, Abdulahi Ali amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akikiri kwamba ni kweli wapiganaji hao waliingia katika hoteli hiyo ambayo imezingirwa na maafisa wa polisi na kwamba milio ya risasi imesikika. Wabunge kadhaa walikuwa ndani ya hoteli hiyo na mmoja wao Mohamed Hassan ameiambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu, kwamba wabunge 10 wameuawa kwa kuchinjwa. Mfanyakazi aliyefaulu kuhepa kutoka katika jengo hilo amesema mmoja wa washambuliaji hao alikuwa mripuaji wa kujitoa mhanga.

Kundi la al-Shabaab limetangaza vita dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.Picha: AP

Wakati huo huo, kiasi ya watu 29 wengi wao wakiwa raia wamaeuawa katika vita mjini Mogadishu baada ya wapiganaji wa kiislamu kutangaza ‘vita vya mwisho’ dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.

Kundi la al-Shabaab lenye msimamo mkali wa kidini linapigana kuipindua serikali dhaifu inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi na inayodhibiti maeneo machache ya mji mkuu, Mogadishu yanayolindwa na kiasi ya wanajeshi 6000 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika wanaotoka Uganda na Burundi.

Ali Muse ambaye ni mkuu wa huduma ya magari ya kuwabeba wagonjwa mjini Mogadishu amesema waathiriwa wanaongezeka kila dakika na vita vinatokota. Aliiambia shirika la habari la Kijerumani, DPA kwamba watu 97 wamejeruhiwa.

Vita vilitokota jana baada ya msemaji wa kundi la al-Shabaab, Sheikh Ali Mohamoud Rage alipotoa amri kwa Waislamu wote nchini Somalia na wapiganaji wa al-Shabaab waingie katika vita ili kuwafukuza wanajeshi aliowaita wenye kuiasi dini kuondoka Mogadishu.

Rowda Abdullahi Hersi, mfanyabiashara katika ngome ya wapiganaji wa al-Shabaab katika soko la Bakara alisema walipokuwa wakitoka sokoni, vita vilizidi na kombora moja lililofyatuliwa likawauwa wanawake watano papo hapo.

Serikali imelilaumu kundi la al-Shabaab kwa kuvurumisha makombora katika maeneo yanayokaliwa na watu wengi, ikisema kwamba kundi hilo halionyeshi heshima katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

Umoja wa Afrika kwa upande wake umeapa kuwaondoa wapiganaji wa kundi hilo la waasi kutoka katika mji mkuu wa Mogadishu. Naibu mwakilishi wa Umoja huo, Wafula Wamunyinyi aliwaambia waandishi wa habari mjini Nairobi kwamba wanajeshi 2000 walioombwa na Jumuiya ya kiserikali ya maendeleo katika pembe ya Afrika, IGAD tayari wameanza kuwasili mjini Mogadishu. Bw Wamunyinyi alisema Guinea na Burundi zinatarajiwa kutuma wanajeshi wa ziada.

Vita vya sasa ambavyo vimesababisha vifo vya kiasi yaw a 20,000, vilianza mwaka wa 2007 kufuatia uvamizi wa Ethiopia ulionuia kuiondoa utawala wa kiislamu. Bw Wamunyinyi alisema ghasia hizo zinawahusisha wapiganaji kutoka Afghanistan na Pakistan.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters/ DPA

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW