1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wa Peshmerga waelekea Kobane kupambana na IS

Admin.WagnerD29 Oktoba 2014

Wapiganaji wa kikurdi wa Iraq wanaojulikana kama Peshmerga wamewasili mapema leo asubuhi kusini mashariki mwa Uturuki tayari kuelekea mjini Kobane nchini Syria kuwasaidia wakurdi wenzao kupambana na wanamgambo wa IS

Picha: AFP/Getty Images/Safin Hamed

Ndege ya Uturuki iliyowabeba wapiganaji hao imetua leo asubuhi katika mji wa Sanliurfa chini ya ulinzi mkali na msafara wa mabasi meupe yaliyosindikizwa na magari ya kijeshi na ya polisi yaliondoka kutoka uwanja wa ndege muda mfupi baadaye.

Kundi jingine la wapiganaji wa kikosi hicho cha Peshmerga wanaaminika kutumia usafiri wa barabarani kuufikia mji huo.Kituo cha televisheni cha kikurdi kimeonyesha picha za msafara wa magari yaliyosheheni silaha nzito yakeielekea katika mji huo wa Uturuki ili kujiandaa kuingia Kobane.

Waasi wa Syria pia waingia Kobane

Duru kutoka Uturuki pia zinaarifu kuwa kundi la wapiganaji 150 wa kundi la waasi la Free Syrian Army FSA leo limevuka kutoka Uturuki na kuingia Syria kuwasaidia wapiganaji wa kikurdi kukabiliana na IS wakitumia magari manane katika kivuko cha mpakani cha Mursitpinar.

Wapiganaji wa kikurdi wa Peshmerga wakielekea KobanePicha: Reuters/Ari Jalal

Afisa wa Uturuki ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema waasi hao wa FSA waliingia Syria usiku wa kuamkia leo. Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria limethibitisha taarifa hizo lakini limesema ni waasi hamsini walioingia Kobane.

Mji wa Kobane ambao uko mpakani kati ya Syria na Uturuki umeshambuliwa vikali na wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS kwa zaidi ya mwezi mmoja na hatma yake imekuwa mtihani mkubwa kwa mkakati wa kijeshi unaoongozwa na Marekani na washirika wake wa kuwakabili wanamgambo hao wa kisunni.

IS imetishia kuwaua wanaojaribu kuulinda mji wa Kobane na kusababisha kiasi cha wakaazi laki mbili wa kikurdi kuutoroka mji huo na kukimbilia nchi jirani ya Uturuki huku wito ukiongezeka wa kuwapa silaha zaidi wapiganaji wa kikudri katika kanda hiyo kukabiliana vilivyo na IS.

Uturuki ambayo imekuwa Ikishinikzwa na Marekani kusaidia katika mapambano dhidi ya IS, wiki iliyopita ilitangaza itaruhusu kiasi cha wapiganaji 150 wa kikurdi kutoka Iraq kupitia nchini mwake na kujiunga na vita vya kuuokoa mji wa Kobane.

Marekani inaendeleza mashambulizi

Marekani imekuwa ikitumia mashambulizi ya angani karibu na Kobane kuwasaidia wapiganaji wa kikurdi kuwazuia wanamgambo wa kundi hilo la dola la kiislamu dhidi ya kuudhibiti mji huo na jeshi la Marekani limesema lilifanya mashambulizi manne juzi na jana na mashambulizi mengine tisa nchini Iraq dhidi ya IS.

Mashambulizi yaliyochacha KobanePicha: Reuters/Yannis Behrakis

Wakati huo huo,wizara ya ulinzi ya Marekani imesema video ya propaganda iliyotolewa hivi punde na wanamgambo wa IS ikimuonyesha mateka wa Kiingereza akijifanya kuwa mwandishi habariwa IS nchini Syria inaonyesha ni jinsi gani kundi hilo lilivyo potovu.

Huku hayo yakijiri, shirika la kutetea haki za binadamu la Syria leo limesema wanamgambo wa IS wameshambulia viwanja vya mafuta na gesi nchini humo na kuwaua wapiganaji na walinzi 30 wanaoiunga mkono serikali ya Syria.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema idadi isiyojulikana ya wanamgambo wa IS pia waliuawa katika mashambulizi hayo yaliyofanyika katika mji wa Shaer katika jimbo la Homs.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW