1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji washirika wa Urusi wauawa nchini Syria

Isaac Gamba
16 Februari 2018

Kiasi ya watu 300 wanaofanya kazi katika kampuni binafisi ya ulinzi yenye mafungamano na ikulu ya Urusi  Kremlin ama waliuawa au kujeruhiwa nchini Syria wiki iliyopita. Ni kwa mujibu wa daktari mmoja wa kijeshi wa Urusi.

Syrien U.S. Air Force A-10 Thunderbolt II Während der Operation Inherent Resolve
Picha: picture alliance/ZUMAPRESS/M. Battles

Muda zilipotolwa taarifa za vifo hivyo unawiana na  mapigano ya Februari 7, karibu na mji wa Deir al-Zor nchini Syria ambako kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na washirika  wa wapiganaji waliohusika , majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani yalishambulia vikosi vinavyoshirikiana na Urusi ambayo ni mshirika wa rais wa Syria  Bashar al- Assad.

Maafisa wa Urusi wanasema raia watano wanaweza kuwa waliuawa lakini hawana mahusiano na vikosi vya urusi.

Mapambano hayo yanaonesha kuwa Urusi inajihusisha zaidi kijeshi nchini Syria  kuliko inavyosema  na kuna uwezekano ikaingia katika makabiliano na Marekani nchini Syria.

Idadi hiyo ya vifo ndiyo kubwa zaidi katika mapambano ya mara moja tangu wakati wa mapambano makali nchini Ukraine mwaka 2014 yaliyosababisha vifo vya wapiganaji 100.   Hata hivyo Urusi imekuwa ikikanusha  kupeleka wanajeshi na wapiganaji wa kujitolea nchini Ukraine na haijawahi kuthibitisha idadi hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo vitano vya habari , majeruhi wamesafirishwa kutoka nchini Syria katika siku chache zilizopita  na kupelekwa kwenye hospitali nne za kijeshi nchini Urusi.

Hali za majeruhi ni mbaya

Mmoja wa wanajeshi wa Urusi waliouawa nchini SyriaPicha: Reuters/Russian Defence Ministry/V. Savistky

Daktari wa kijeshi anayefanya kazi  katika hospitali ya kijeshi mjini Moscow na ambaye  alihusika moja kwa moja  na matibabu ya waliorejeshwa kutoka nchini Syria  amesema kufikia Jumamosi iliyopita kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 katika hospitali anayofanya kazi  huku asilimia 30 hali zao zikiwa ni mbaya .

Daktari huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwasababu haruhusiwi kuzungumzia  taarifa hizo amesema kiasi cha ndege tatu zilizokuwa zimewabeba  majeruhi wapiganaji zilitua mjini Moscow kati ya Ijumaa na Jumatatu  asubuhi wiki hii.

Amesema walirejeshwa kwa kutumia ndege maalumu za mizigo zenye vifaa maalumu vya kitabibu kwa ajili ya kutoa huduma  za dharula ambazo zilikuwa na majeruhi kadhaa.

Maria Zakhrova  msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi amesema taarifa za awali zinaonesha kuwa raia watano wa Urusi wanaweza kuwa wameuawa katika uwanja wa mapambano lakini hawakuwa wanajeshi wa Urusi na kusisitiza kuwa  taarifa kwamba makumi au mamia wameuawa  ni taarifa za kupotosha ambazo zinatolewa na wapinzani wa Urusi.

Wizara ya ulinzi ya Urusi haikujibu maswali ya shirika la habari la Reuters kuhusiana na idadi ya waliouawa nchini Syria na msemaji wa ikulu ya Urusi , Kremlin alipoulizwa kuhusiana na vifo hivyo alisema hana la kuongeza tofauti na taarifa za awali.

Ikuru ya Urusi imesema mapema wiki hii kuwa haina taarifa zozote kuhusiana na vifo hivyo.

Shirika la habari la Reuters halikufanikiwa kufanya mawasiliano ya moja kwa moja  na waajiri wa wakandarasi hao wa ulinzi, kampuni ijulikanayo kama "Wagner  Group" ambao wapiganaji wake wamewahi katika siku zilizopita kupokea medali kutoka ikulu ya Kremlin.

Daktari wa kijeshi amesema daktari mwenzie aliyekwenda nchini Syria  hivi karibuni alimueleza kuwa  kiasi ya watu 100 katika jeshi la Urusi wameuawa katika kipindi cha wiki iliyopita na wengine 200 wamejeruhiwa.

Mwandishi : Isaac Gamba/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW