Wapiganaji wateka mji mwingine Iraq
16 Juni 2014Meya wa mji wa Tal Afar Abdulal Abdoul amethibitisha kuanguka kwa mji huo wa wakaazi wapatao laki mbili, wengi wao wakiwa Washia na Wasunni wenye asili ya Uturuki, kabla ya Alfajiri.
Mkaazi wa mji huo Hadeer Al-Abadi aliezungumza na shirika la habari la Associated Press kwa njia ya simu, alithibitisha pia kuanguka kwa mji huo, na kusema vikosi vya usalama viliondoka kabla ya Alfajiri, na kwamba wakaazi wengi wamejawa na hofu na wengi wameukimbia mji huo.
Kuanguka kwa Tal Afar kunakuja wiki moja baada ya wapiganaji hao wa kisunni kuuteka mji wa pili kwa ukubw anchini Iraq wa Mosul, na mji wa nyumbani kwa rais wa zamani Saddam Hussein wa Tikrit.
Maliki aapa kurejesha kila inchi iliyotekwa
Kutekwa kwa mji huo pia kumekuja saa chache baada ya waziri mkuu Nouri al-Maliki, akizungumza na raia waliojitolea kujiunga na vikosi vya usalama, kuapa kurejesha kila inchi ya ardhi iliyochukuliwa na wapiganaji hao, na msemaji wa jeshi la Iraq Luteni Jenerali Kassam Al-Mussawi, akielezea mafanikio yaliyopatikana dhidi ya wapiganaji hao katika siku chache zilizotangulia.
"Vikosi vyetu vya usalama vimepata tena hamasa ya kufanya mashambulizi bora katika maeneo tofauti katika kipindi cha siku tatu zilizopita na vimepata mafanikio muhimu kwa msaada wa raia waliojitolea," alisema Luteni Jenerali Mussawi.
Mwishoni mwa wiki, wapiganaji waliweka picha kwenye mitandao, ambazo ziliwaonyesha baadhi yao wakiwauwa wanajeshi wa Iraq waliotekwa. Luteni Jenerali Mussawi alisema tathmini ya picha hizo na wataalamu w akijehsi ilionyesha kuwa karibu wanajeshi 170 waliuawa.
Onyo dhidi ya vita vya uwakala
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki alisema madai hayo ya wapiganaji ni ya kuogofya, huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akisema waliohusika na unyama huo laazima wakabiliwe na mkono wa sheria.
Wakati hayo yakijiri, waziri wa mambo ya kigeni wa Qatar Khaled al-Attiyah, amemtuhumu waziri mkuu Nouri al-Maliki kwa kusababisha machafuko ya sasa kutokana na sera zake za kuwatweza wasunni wachache, tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa Iraq Saddam Hussein mwaka 2003.
Uhusiano kati ya Iraq na Qatar ni wa mashaka. Mwezi Machi Maliki aliituhumu Qatar pamoja na Saudi Arabia kwa madai ya kuunga mkono ugaidi. Siku ya Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliyaonya mataifa ya kanda hiyo dhidi ya kuanzisha vita alivyoviita vya uwakala nchini Iraq.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman