Wapinzani kushikiri mazungumzoya amani ya Syria
13 Februari 2017Hapo kabla makundi hayo yamekuwa yakikosoa makundi yenye silaha kwa kupambana na utawala wa rais bashar al-Assad.
Kamati kuu ya majadiliano , HNC ikiwa ni chombo kinajumuisha makundi mengine madogo madogo , imesema katika taarifa baada ya siku mbili za majadiliano mjini Riyadh nchini Saudi Arabia , kwamba kikundi hicho chenye wanachama 21 watakaoshiriki katika majadiliano ni pamoja na makundi wanachama mawili ya muungano wa wapiganaji ambao hapo kabla walikuwa wanapingana.
Muungano wa makundi hayo mawili, lile linalofahamika kama makundi ya Moscow na Cairo , kwa muda mrefu yamekuwa yakipinga mapigano ya waasi na kusisitiza kwamba mabadiliko ya kisiasa yanaweza tu kupatikana kupitia harakati za amani. Wanachama wao ni pamoja na waziri wa zamani wa serikali ya Syria akiwa na mahusiano ya karibu na Urusi.
Mohammad Sabra , ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa majadiliano, alikiambia kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Saudi Arabia cha Al-Hadath kwamba ujumbe huo umeyaleta pamoja makundi mbali mbali.
Mataifa ya kigeni
Pia ameyashutumu mataifa ya kigeni yenye nguvu ambayo hakuyataja kwa kujaribu kulazimisha mawazo yao juu ya muundo wa ujumbe huo, akimaanisha Urusi.
Chombo hicho pia kilimchagua kiongozi wao mkuu mpya atakayeongoza majadiliano, Nassir al-Hariri, mpinzani maarufu akitokea kusini mwa Syria.
Duru ijayo ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na mzozo huo, ukiwa sasa katika mwaka wake wa sita , imepangwa kuanza Februari 20.
Kundi la HNC limesema katika taarifa kwamba lengo la majadiliano hayo ni kupata suluhisho la kisiasa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa ambapo Assad hatakuwa na jukumu katika hatima ya nchi hiyo. Lakini kundi hilo limejitoa kutoka katika msimamo wao wa hapo kabla kwamba rais wa Syria analazimika kujiondoa kabla ya kuanza kwa awamu ya mpito.
Mswada wa katiba
HNC pia limesema mataifa ya nje yenye nguvu hayana haki ya kuweka mtazamo wao kuhusiana na mfumo wa kisiasa wa hapo baadaye nchini Syria. Urusi mwezi uliopita iliwasilisha mswada wa katiba mpya inayopendekezwa kwa ajili ya Syria, licha ya kusisitiza kwamba waraka huo umesambazwa kwa madhumuni ya majadiliano tu.
Wakati huo huo serikali ya Syria imesema leo kwamba iko tayari kukubaliana kubadilishana mateka wa vita , hatua muhimu ya kujenga hali ya kuaminiana wakati Umoja wa Mataifa ukijitayarisha kuitisha mazungumzo mapya ya amani.
Upinzani nchini Syria umekuwa ukidai kwa muda mrefu kuachiliwa kwa wafungwa wanaoshikiliwa na serikali kama moja kati ya hatua kadhaa za kibinadamu wanasema ni lazima zifanyike kabla ya majadiliano yoyote kuhusiana na hali ya baadaye ya kisiasa nchini Syria.
Nayo majeshi ya Syria yamesogea karibu kilometa 20 kuelekea mji wa Palmyra katika juhudi za kuukomboa mji huo wa kale kutoka kwa kundi la waasi la Dola la Kiislamu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu