1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Tanzania walalamikia 'rafu' uchaguzi mkuu

29 Oktoba 2020

Mgombea wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzani, Chadema Tundu Lissu, amedai kuwa uchaguzi, ulikumbwa na kasoro, huku baadhi ya waangalizi wakisema nchi hiyo inakabiliwa na miaka mitano mingine ya utawala wa kimabavu.

Bildkombo Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli und Tundu Lissu

Matokeo yanayotangazwa na tume ya uchaguzi hayawezi kupingwa mahakamani, jambo linalotilia umuhimu wa juhudi za usimamizi wa kura, lakini upinzani ulisema wasimamizi wake walitimuliwa kutoka vituo kadhaa vya kupigia kura. Baadhi ya wangalizi huru kama Umoja wa Ulaya hawakualikwa au walizuwiwa, tofauti na chaguzi zilizopita.

Mgombea wa chama kikuu cha upinzani Chadema, Tundu Lissu, alisema hatua kubwa za kidemokrasia ndiyo njia pekee ya kulinda uaminifu wa uchaguzi. Manusura huyo wa jribio la mauaji la mwak 2017, alirejea, kutoka nje ya nchi mwaka huu kushindana na rais John Magufuli, anaewania muhula wa pili.

Soma pia: Zoezi la kuhesabu kura laanza Tanzania

Chama kingine kikubwa cha upinzani cha ACT Wazalendo, kilichoripoti vurugu mbaya kabla ya kura hiyo, kilisema mawakal wake wa uchaguzi walishuhudia masanduku ya kura yakinyakuliwa na maafisa wa usalama, mengine yakijazwa kura zilizopigwa tayari na wapiga kura wengine waliorudishwa na maafisa waliosema kwamba karatasi za kura zimeisha.

Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.Picha: Ericky Boniphace/DW

Katika visiwa vya Zanzibar vyenye mamlaka yake ya ndani, chama cha ACT Wazalendo kilidai kwenye taarifa kwamba mwanaume mmoja alijitokeza na kitambulisho cha mtu aliekufa.

Mtoto wa kiume wa marehemu huyo hata hivyo, alikuwepo ktika kituo cha kupigia kura kama wakala wa chama hicho, na kwamba wakala huyo alifurushwa kutoka kituoni hapo na mamluki huyo aliruhusiwa kupiga kura. 

Afisa wa chama cha ACT Wazalendo Ismail Jussa, aliutaja uchaguzi wa jana kuwa mbaya zaidi katika historia ya Tanzania, wakati akizungumza na shirika la habari la Associated Press.

Soma pia: Uchaguzi Tanzania: Wagombea wapiga kura

Alisema polisi ilimuamuru kutoka nje alipojaribu kushuhudia zoezi la kuhesabu kura, na kisha akaona vifaru mitaani wakati akiendesha gari kurudi kwenye ofisi za chama chake. 

'Mtu mmoja kura hadi 20'

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Muhene Said Rashid, alisema waligundua watu waliokuwaa na karatasi nyingi za kura katika vituo mbalimbali.

"Mtu mmoja anapewa labda karatasi kumi au kumi na tano au hadi 20 na kuna baadhi ya watu waliokuja leo asubuhi kuripoti kwetu kwamba walipewa kura kumi kuzipiga kwa wakati mmoja," alisema Rashid.

Wapiga kura wakiwa kwenye foreni wakisubiri kutekeleza haki yao ya kikatiba.Picha: Ericky Boniphace/DW

Hata kabla ya mapambazuko, baadhi walidai kutishiwa, akiwemo mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe, alieweka ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter akielezea kwamba maisha yake yako hatarini, na baadae akatoa picha za mkanda wa vidio ya uchunguzi, ambayo alisema ilionesha afisa wa serikali aliekuwa na silaha akiwa nje ya hoteli yake.

Soma pia:Mawakala wa upinzani washindwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura 

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Semistocles Kaijage, alisema katika taarifa baada ya uchaguzi kwamba madai yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kuwepo na kasoro kwenye zoezi la uchaguzi hayakuwa na ukweli wowote, na kuongeza kuwa tume ya uchaguzi ilisema haikupokea taarifa yoyote rasmi juu ya madai ya udanganyifu.

Taifa hilo limegeuka mzozo wa kibinadamu, wakati ambapo wanadiplomasia, Umoja wa Mataifa na wengine wakisema serikali ya rais Magufuli imeminya uhuru wa vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na sauti za upinzani. Pia anashutumiwa kwa kupuuza hatari ya janga la virusi vya corona, kwa kudai kwamba Tanzania imelishinda janga hilo kupitia sala.

Maoni Tanzania Masaa 48 kuelekea uchaguzi mkuu

02:10

This browser does not support the video element.

Soma pia: Dk Ali Mohammed Shein aagwa baada ya miaka 10 uongozini

Rais Mafuguli ambaye alisisitiza haja ya kutunza amani baada ya kupiga kura yake jana, amejizolea sifa kwa sehemu kutokana na kupiga vita rushwa, kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuimarisha uchumi wa taifa hilo, ambao ni mmoja ya chumi zinazokuwa kwa kasi kubwa zaidi barani Afrika. Yeyote atakaepata kura nyingi zaidi atashinda bila kuwepo na duru ya pili.

Huduma za mawasiliano ya intanet zilikuwa chini au hazipatikani kabisaa siku ya Jumatano, na waandishi habari wachache tu wa kigeni walipata idhini ya kuripoti uchaguzi huo kutokea ndani ya Tanzania.

Kulikuwa na uwepo mkubwa wa vikosi vya polisi na jeshi visiwani Zanzibar, siku moja baada ya chama cha ACT Wazalendo kulituhumu jeshi la polisi kwa kuwauwa kwa risasi watu tisa, tuhuma ambazo polisi ilikanusha.

Vyanzo: AP, AFPTV

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW