1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani waandamwa Burundi, linasema Human Rights Watch

Oumilkheir Hamidou
13 Juni 2019

Maafisa wa serikali ya Burundi na vijana wa Imbonerakure wanahusika na kupigwa,kukamatwa kiholela, kupotea na kuuwawa wapinzani tangu wa kweli mpaka wanaodhaniwa.Shirika la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake

Archivbild - Burundi's President Pierre Nkurunziza
Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Kampeni ya kuwaandama watu wanaotuhumiwa kukipinga chama tawala imekuwa ikiendelea tangu kura ya maoni ya katiba ilipoitishwa Mei mwaka jana. Hata hivyo kampeni hiyo inaonyesha kuzidi makali tangu chama kipya cha upinzani kiliposajiliwa mwezi wa Februari mwaka huu.

Wanachama wa Imbonerakure, jumuiya ya vijana wanaoshirikiana na chama tawala cha CNDD-FDD na wakuu wa serikali za mikoa wanaendelea kuwashinikiza raia na hasa wa mashambani wajiunge na chama tawala mnamo wakati huu ambapo Burundi inajiandaa kwa uchaguzi wa rais mwaka 2020.  Shirika la Human Rights Watch linasema katika ripoti yake vijana wa Imbonerakure na viongozi wa serikali za mikoa wanawaandama wanachama wa chama kipya cha "Baraza la taifa kwa ajili ya Uhuru-CNL katika mikoa isiyopungua minane kati ya 18 bila ya kuhofia adhabu yoyote.

Vikosi vya polisi nchini Burundi vilipoifunga ofisi ya shirika la haki za binaadam la Umoja wa mataifa mjini Bujumbura mei 26 mwaka 2015Picha: picture alliance/dpa/D. Kurokawa

 Visa vilivyoripotiwa ni sehemu ndogo tu ya visa jumla

Lewis Mudge, mkurugenzi wa Human Rights Watch kwa eneo la Afrika Kati anasema matumizi ya nguvu yanayozidi kukithiri yamesababishwa na hali ya watu kutojali sheria ikiyoko nchini Burundi. Anavitaja visa vilivyoripotiwa kuwa ni sehemu ndogo tuu ya visa vinavyotokea na ambavyo haviripotiwi kutokana na kutokuwepo vyombo huru vya habari na mashirika ya kijamii.

Kati ya mwezi wa Februari hadi Mei mwaka huu shirika la Human Rights Watch limefanya mahojiano 33 kwa njia ya simu pamoja na wahanga, familia zao na mashahidi wa visa vilivyotokea katika mikoa ya Babanza, Cibitoke, Gitega, Karusi, Kirundo, Muramvya, Muyinga, Ngozi na Rumonge pamoja pia na katika mji mkuu Bujumbura. Zaidi ya hayo wachunguzi wa shirika hilo linalopigania haki za binaadam wamewahoji watu 30 walioipa kisogo Burundi baada ya kura ya maoni ya Mei mwaka jana.

Visa visivyopungua vitatu vya mauwaji, vinne vya watu wasiojulikana waliko na 24 vya watu waliokamatwa kiholela vimeorodheshwa na Human Rights Watch katika mikoa hiyo minane ya Burundi tangu Januari mwaka huu. Zaidi ya hayo kuna kadhia za mauwaji ya watu 3 na mmoja ambaye hajulikani aliko zilizoripotiwa na shirika hilo la haki za binaadam baada ya Mei 2018 nchini Burundi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kesho kuzungumzia hali inayozidi kua mbaya nchini Burundi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Human Rights Watch

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW