1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waranti wa kukamatwa kwa Puigdemont watolewa

4 Novemba 2017

Makahama Kuu ya Uhispania imetoa waranti wa kukamatwa kwa aliyekuwa kiongozi wa jimbo la Catalonia, Carles Puigdemont, aliyekimbilia Ubelgiji baada ya kuvuliwa madaraka kwa kutangaza uhuru wa Catalonia kutoka Uhispania.

Spanien Katalonien Rede Carles Puigdemont
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Morenatti

Jaji wa Mahakama Kuu ya mjini Madrid Carmen Lamela ameitaka Ubelgiji kumkamata Puigdemont na washirika wake wanne baada ya kudharau amri ya mahamaka iliyowataka warudi Uhispania Alhamisi iliyopita ili kujibu mashtaka ya uasi, matumizi mabaya ya fedha za umma, kutotii amri pamoja na uvunjaji wa uaminifu yote yakihusishwa na kampeni yao ya kutaka kujitenga.

Mwendesha mashitaka wa Ubelgiji Eric Van der Sypt amesema wamepokea waranti huo wa kukamatwa kwa Puigdemont na waliokuwa mawaziri wanne wa Catalonia na kuongeza itachunguza waranti huo na kuuwasilisha kwa jaji katika siku chache zijazo.

Ubelgiji itachukua hatua gani?

Ubelgiji ambako waranti wa kukamatwa wa Ulaya huenda ukazuiwa kwa sababu kadha wa kadha, itakuwa na hadi miezi mitatu kuamua iwapo itamrejesha au la Puigdemont nchini mwake. Jaji wa mahaka ya juu wa Uhispania alikataa ombi la Puigdemont kutoa ushahidi wake kupitia mawasiliano ya video kutoka Ubelgiji.

Waliokuwa viongozi wa Catalonia wakiwasili mahakamaniPicha: REUTERS

Puigdemont, anayetarajia kushiriki katika uchaguzi wa mapema wa Desemba 21, amesema hauamini mfumo wa haki wa Kihispania lakini atashirikiana na mahakama ya Ubelgiji.

Saa chache kabla ya waranti huo kutolewa kiongozi huyo alisema yuko tayari kujisalimisha kwa maafisa wa Ubelgiji iwapo waranti wa kukamatwa kwake utatolewa na Uhispania.

Puigdemont ameapa kufanya kampeni kuelekea uchaguzi wa mapema jimboni mwake uliotishwa na serikali kuu ya Uhispania akiwa nchi ya kigeni, akihoji anaweza kufanya hivyo kwasababu wanaishi katika ulimwengu wa utandawazi, huku akilaani kile alichokitaja vitendo vya kinyama vinavyofanywa na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy.

Siku ya Alhamisi, mahakama ya Uhispania iliamuru viongozi wanane wa serikali iliyovunjwa ya Catalonia kuzuiwa bila ya dhamana akiwemo aliyekuwa makamu wa Rais wa Oriol Junqueras.

Rajoy azidi kukaza kitanzi

Serikali kuu ya Uhispania iliwavua madaraka viongozi wa Catalonia muda mchache baada ya bunge la jimbo hilo tajiri kupiga kura kuidhinisha kujitenga na kujitawala mnamo tarehe 27 Oktoba.

Waziri mkuu wa Uhispania Mariano RajoyPicha: Reuters/S. Vera

Wakati huo huo, makundi yanayounga mkono Catalonia kuwa taifa huru lijulikanalo Asamblea Nacional Catalana ANC na Omnium yameitisha maandamano ya umma kupinga kukamatwa na kuzuiwa kwa viongozi wa iliyokuwa serikali ya jimbo la Catalonia.

Viongozi wa makundi hayo walifungwa jela mwezi uliopita kwa mashtaka ya kuchochea uasi.

Maelfu ya Wacatalonia waliandama Alhamisi usiku katika miji kadha jimboni humo, na vyama vinavyounda muungano wa Junts Pel Si vimetangaza vitawania kwa pamoja katika uchaguzi huo wa Desemba.

Uchunguzi wa utafiti wa maoni ya wapiga kura unaonyesha kuwa Junts Pel Si utashinda kwa asilimia 35.2 ya kura na huenda ukawa na wingi wa viti bungeni iwapo utaendelea kuwa pamoja na mshirika wake wa sasa, chama cha mrengoo wa kushoro cha CUP.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/Reuters/ap

Mhariri: Yusra Buwayhid