1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warundi waandamana kupinga jeshi la kulinda amani

26 Desemba 2015

Wafuasi wanaoiunga mkono serikali Jumamosi (26.12.2015) wameandamana nchini kote Burundi dhidi ya mipango ya Umoja wa Afrika kutuma wanajeshi 5,000 wa kulinda amani nchini humo

Bujumbura Burundi Protest Gewalt
Picha: picture-alliance/D. Kurokawa

Umoja wa Afrika ulitangaza wiki iliopita kwamba inapanga kutuma wanajeshi hao wa kulinda amani ili kuzuwiya machafuko zaidi nchini humo ambapo waandamanaji wamekuwa wakipinga hatua ya Rais Piere Nkurunziza kubakia madarakani kwa muhula wa tatu.

Maandamano ya Jumamosi yamefanyikka kwenye miji mikubwa ilioko katika majimbo 18 ambapo waandamanaji mjini Bujumbura walikuwa na mabango yenye kusema "Tunapinga uwekaji wa wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Burundi" na "Hakuna vita au mauaji ya kimbari kuhalalisha uwekaji wa wanajeshi wa Umoja wa Afrika".

Makamo wa Rais Gaston Sindimwo akizungumza katika maandamano yaliohuhduruwa na mamia ya watu mjini Bujumbura amesema "Hakuna askari wa kigeni akayekanyaga ardhi ya Burundi bila ya idhini ya serikali." Amewaonya wanasiasa ambao wanavuruga usalama wa Burundi kwamba hawatowavumilia na kwamba wataendelea kupambana na wahalifu.

Umoja wa Afrika umesema kikosi cha awali kilichopangwa kutumwa nchini humo kitakuwa na mamlaka ya kuzuwiya vitendo vyoyote vinavyofanya hali ya usalama kuzidi kuwa mbaya na kuchangia kuwalinda raia walioko hatarini.

Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika limesema Ijumaa usiku kwamba iwapo Burundi haitokubali uwekaji wa vikosi hivyo katika kipindi kisichozidi saa 96 wanajeshi hao wa kulinda amani watatumwa nchini humo kwa itakavyokuwa hata dhidi ya matakwa ya serikali.

Jeshi la Kulinda amani la Afrika nchini SomaliaPicha: picture alliance/AP Photo/Jones

Umoja wa Afrika umesema shughuli zake hizo pia zinakusudia kurahisisha mchakato wa kisiasa kutatuwa mzozo wa kikabila unaozidi kukuwa kati ya Wahutu na Watutsi.

Kwa mujibu wa umoja huo mtu yoyote yule atakayepinga uwekaji wa vikosi vyake hivyo atakabiliwa na vikwazo na hivi sasa asasi hiyo inatafuta namna ya kugharamia uwekaji wa vikosi vyake hivyo.

Kiongozi wa Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini -Zuma amejaribu kuihakikishia Burundi kwamba mpango wake huo wa kupeleka wanajeshi nchini humo unakusudia kukomesha machafuko yaliodumu kwa miezi kadhaa kwa njia ya amani na hawana agenda yoyote ile ya siri dhidi ya nchi hiyo.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa chombo hicho kutumia nguvu kuweka wanajeshi katika nchi mwanachama wake bila ya ridhaa ya nchi husika Burundi ambayo inasema pendekezo hilo la kutuma wanajeshi linakiuka uhuru wa nchi hiyo.

Kuna wasi wasi mkubwa kwamba Burundi inaweza kutumbukia kwenye vita vyengine vya kikabila kati ya Wahutu na Watutsi.

Umoja wa Mataifa umesema mwezi huu amba nchi hiyo yenye wakaazi milioni 11 iko kwenye ukingo wa vita vyengine vya wenyewe kwa wenyewe ambapo tayari watu 250,000 wamekimbilia nchi jirani.

Nkurunziza ameuchochea mzozo huo wakati alipotangaza hapo mwezi wa Aprili kwamba angeligombania urais kwa muhula mwengine wa tatu.

Vita vya karibuni kabisa vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ya kimaskini kati ya Wahutu na Watutsi kufuatia mauaji ya kimbari ya nchi jirani ya Rwanda hapo mwaka 1994 vilimalizika mwaka 2005 na kuuwa watu 300,000.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters
Mhariri: Bruce Amani