Warundi wanaendelea kuikimbia nchi yao
25 Agosti 2017Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Kimataifa ya Haki za Wakimbizi, IRRI, ambayo inaeleza kuwa wafuasi wa kundi la vijana wa chama tawala nchini Burundi, Imbonerakure wanaendelea kufanya mauaji na kuwalazimisha kupotea wale ambao wanawaona kama wanaipinga serikali.
Taasisi ya IRRI inaeleza kuwa ushahidi uliokusanywa kutoka kwa wananchi wa Burundi waliowasili Uganda kati ya mwezi Machi na Juni mwaka huu wa 2017, unakinzana na wito rasmi wa serikali ambao unawataka wakimbizi warejee nyumbani kwa sababu amani na usalama vimerejea nchi humo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa huku kweli baadhi yao wakirejea Burundi, idadi mpya ya wakimbizi wanaoikimbia nchini humo kwenda kwenye nchi za jirani, kwa kiasi kikubwa inaizidi ile ya wanaorejea nyumbani.
Thijs Van Laer, Meneja Mipango wa IRRI, anasema kuwa wakimbizi wamekuwa wakisimulia mambo mabaya ambayo wanafanyiwa ikiwemo ubakaji, kuteswa na mauaji ambayo yanafanywa na Imbonerakure pamoja na vikosi vya usalama vya Burundi, wakiwalenga hasa wafuasi wa upinzani, lakini pia wananchi wa kawaida.
Ripoti inafafanua kwamba ikiwa serikali ya Burundi kweli inataka kuwahamasisha wakimbizi warejee nyumbani, lazima walizuie kundi la Imbonerakure na ihakikishe kuwa wanawajibishwa kutokana na unyanyasaji walioufanya tangu kuanza kwa mzozo wa kisiasa, ikiwemo wakati wa ushirikiano wa juhudi za kimataifa.
Mzozo wa kisiasa uliibuka 2015
Burundi ilitumbukia katika mzozo wa kisiasa Aprili mwaka 2015, wakati ambapo Rais Pierre Nkurunziza alitangaza nia yake ya kugombea urais kwa awamu ya tatu, ambapo aligombea na kushinda.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kiasi ya watu 500 wameuawa katika ghasia, ingawa mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanasema idadi ya watu waliouawa ni zaidi ya 1,000 na wengine zaidi ya 400,000 wameikimbia nchi hiyo tangu mzozo huo ulipozuka.
Rais Nkurunziza alizuru Tanzania mwezi Julai mwaka huu katika ziara isiyo ya kawaida, ambapo alitangaza kuwa Burundi sasa ina amani na kuwatolea wito wakimbizi warejee nyumbani.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, limesema kuwa wananchi 275,000 wa Burundi walikimbilia Tanzania, idadi ambayo inapingwa na serikali zote mbili na kusisitiza kuwa idadi kubwa ya wakimbizi tayari wamerejea nyumbani.
Kwa mujibu wa UNHCR, Rwanda ambayo inawahifadhi zaidi ya wakimbizi 86,000, ikiwa ni idadi ya pili ya juu katika ukanda huo, sasa inapokea wakimbizi 150 wanaoingia nchini humo kwa wiki.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef