Warusi wapiga kura kuchagua bunge bila upinzani mkuu
17 Septemba 2021Hakuna matarajio kwamba chama cha United Russia kitapoteza udhibiti wake wa Duma, ambalo ndilo baraza la kuchaguliwa la bunge la Urusi. Maswali muhimu yanayopaswa kujibiwa ni iwapo chama hicho kitabakisha wingi wake wa sasa wa theluthi mbili, unaokiwezesha kufanya mabadiliko ya kikatiba; iwapo uitikiaji usioridhisha utafifisha hadhi ya chama hicho; na iwapo mkakati wa kiongozi wa upinzani alieko gerezani Alexei Navalny, utathibitisha kuwa sahihi dhidi ya chama hicho.
Kremlin imewaondoa mahasimu wake wengi kwenye kinyanganyiro, kwa kuwafunga gerezani wanachama wengi wa upinzani, kuwazuwia korokoroni au kutowaruhusu kugombea. Wakati huo huo, vyombo huru vya habari vimefungwa kimoja baada ya kingine katika miezi ya karibuni baada ya mamlaka kuvilenga kwa kuviita "mawakala wa mataifa ya kigeni", huku waangalizi wa uchaguzi kutoka shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya , OSCE, halitakuwepo kufuatilia uchaguzi huo.
Kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, anajaribu kutokea gerezani, kupigia debe mkakati wa kile kinachoitwa upigaji kura wa kijanja - ambao ni mkakati ambamo wapigakura wanaoipinga Kremlin wanawaunga mkono kwa wingi wagombea wanaoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuwashinda wabunge wa chama tawala.
Washirika wa Navalny wamebuni programu ya simu na mifumo ya mtandaoni kusaidia Upigaji kura wa Kijanja, lakini athari ya mbinu hiyo kwenye matokeo ya uchaguzi ilikuwa bado kitendawili.
''Nakuombeni mshiriki katika uchaguzi ujao''
Kutokea kambi yake anakozuwiliwa mashariki mwa mji wa Moscow, Navalvy ameweza kufikisha ujumbe kwa wafuasi wake ambamo anawahimiza kushirikiana ili kuuondoa mfumo wa ufisadi wa Putin.
Wachambuzi wanasema kuna msisimko kidogo sana kwenye uchaguzi huu, lakini Rais Putin amewahimiza Warusi kupiga kura, akisema katika ujumbe wa vidio hapo jana, kwamba uchaguzi wa leo bila shaka ndiyo tukio uhimu muhimu zaidi katika taifa hilo.
''Wapendwa marafiki! Nakuombeni mshiriki katika uchaguzi ujao, chagueni kwa hili, siku yoyote inayowafaa, kuanzia Septemba 17, njooni kwenye vituo vya kupigia kura, au tumieni uwezekano wa njia ya upigaji kura ya kielektroniki. Teknolojia za kisasa zinahakikisha usalama na uaminifu wake.'', alisema Putin.
Upigaji kura ulianza mapema leo katika mikoa ya mbali mashariki ya Kamchatka na Chukotka, ambayo ina tofauti ya masaa tisa mbele ya Moscow. Wapigakura wataweza kuendelea kupiga kura zao hadi siku ya Jumapili. Ikulu ya Kremlin inataka kulidhibiti bunge jipya, ambalo litakuwepo bado mwaka 2024, wakati muhula wa sasa wa Putin utakapomalizika, na anapaswa kuamua juu ya kugombea tena au kuchagua mkakati mwingine wa kusalia madarakani.