1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasaidizi wa Biden wafanya mazungumzo na Israel

Angela Mdungu
12 Machi 2021

Maafisa wa Israeli na Marekani, walifanya mazungumzo Alhamisi kwa njia ya video kwa mara ya kwanza kuijadili Iran. Mazungumzo hayo pia yalitawaliwa na masuala mengine ya kieneo

Bildkombo Netanjahu und Joe Biden

Mkutano wa kwanza wa kimkakati kati ya Israel na Marekani kwa njia ya video ulioongozwa na mshauri wa usalama wa taifa Jake Sullivan na mwenzake wa Israeli Meir Ben-Shabbat, umefanyika wakati timu ya usalama wa taifa ya Rais Biden ikiongeza bidii za kuihusisha Israeli kwenye suala la Iran. 

Msemaji wa baraza la usalama la taifa wa Marekani Emily Horne, alisema pande hizo mbili zina mitizamo inayofanana kuhusu masuala ya usalama katika eneo la mashariki ya kati ikiwa ni pamoja na Iran, na wameelezea dhamira yao ya kukabiliana na changamoto na vitisho vinavyolikabili eneo hilo.

Hata hivyo Israeli haijatoa tamko lolote, kuhusiana na mazungumzo yaliyofanyika Alhamisi. Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani  Anthony Blinken kusema katika hotuba yake ya kwanza mbele ya bunge hapo Jumatano kuwa, Rais Biden amedhamiria kushauriana na Israeli na mataifa mengine ya eneo la Ghuba  katika kusonga mbele ili kupata makubaliano na Iran.

Biden anajaribu kuepuka vikwazo kama alivyokabiliana navyo Rais Obama wakati wa kuelekea kusaini mkataba wa nyuklia wa Iran ambapo Iran, ilikubali kuondokana na akiba yake ya madini ya Urani, na kuruhusu ifuatiliwe na Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya Atomiki – IAEA kwa sharti la kupunguziwa vikwazo.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuven Castro/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikosoa makubaliano hayo  ambapo katika moja ya hotuba zake kwa bunge aliziita juhudi za Obama kuwa ni juhudi za "kuuaga udhibiti wa silaha.” Naye Rais Donald Trump, aliyemuona Netanyahu kama mmoja wa washirika wake wa karibu kati ya viongozi wengi wa mataifa ya kigeni, alijitoa kwenye makubaliano hayo, Mei 2018.

Mwezi uliopita, Biden alitangaza kuwa utawala wake uko tayari kujfanya mazungumzo na Iran, pamoja na mataifa mengine yenye nguvu duniani kujadili kurejea katika makubaliano ya mwaka 2015. Iran yashikilia msimamo wa kuondolewa vikwazo

Hata hivyo Iran, imetilia mkazo matakwa yake ya kuondolewa kwa vikwazo ilivyokuwa imewekewa na Trump kabla ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Israel inaiona Iran kama tishio lake kimkakati kwa sababu ya mpango wake wa nyuklia, uungaji wake mkono makundi ya wabeba silaha wa Lebanon na maeneo ya Wapalestina bila kusahau matamshi makali ya viongozi wa Iran ambao mara nyingi wamekuwa wakitabiri anguko la Israeli.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW