1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasaidizi wawili wa Donald Trump hatarini kwenda jela

22 Agosti 2018

Meneja wa zamani wa rais Trump, Paul Manfort amepatikana na hatia kwenye makosa manane kati ya 18 yaliyomkabili kuhusiana na uhalifu wa kifedha na ukwepaji kodi.

Kombi-Bild - USA Russland-Affäre - Donald Trump, Michael Cohen und Stormy Daniels
Picha: picture alliance/AP

Rais wa Marekani Donald Trump amepata pigo mara mbili baada ya wasaidizi wake wawili kupatikana na hatia. Wakili wake binafsi  wa muda mrefu Michael Cohen amekiri kukiuka sheria juu ya matumizi ya fedha za kuendeshea kampeni za uchaguzi, baada ya kufikia mapatano na waendesha mashtaka wa serikali kuu mjini New York. 

Bwana Michael Cohen mwenyewe amekubali makosa ya kutumia fedha za kampeni za uchaguzi kwa ajili ya kumlipa mwanamke mmoja nyota wa filamu za ngono, Stormy Daniels anayedai kuwa aliwahi kutembea na Rais Donald Trump. Hatua ya bwana Cohen kukiri kutenda uhalifu inamuhusisha rais Trump hasa baada ya Cohen kuiambia mahakama kwamba aliagizwa na mjumbe aliyekuwa anawania kiti cha urais, kuwezesha mwanamke huyo alipwe. Inadaiwa kwamba mama huyo alilipwa fedha hizo ili afiche siri kuhusu yaliyotokea kati yake na rais Trump.

Aliyekuwa wakili wa rais Donald Trump, Michael CohenPicha: Getty Images/AFP/T.A. Clary

Kukiri kwa bwana Cohen kunaweza kumlazimu atoe habari zaidi kwa tume maalumu ya Robert Mueller, inayochunguza madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016. Bwana Cohen amesema kwamba aliyekuwa msanii wa mitindo wa jarida la ngono la Playboy Karen McDougal pia alilipwa ili anyamaze kimya. Maseneta wa chama cha Republican wametoa kauli za tahadhari juu ya watu hao waliokuwa wapambe wakubwa wa rais Trump.

Juu ya bwana Michael Cohen kumhusisha rais Trump katika ushahidi aliotoa kwa waendesha mashtaka, wakili wake, Lanny Davis amesema ikiwa Cohen ametenda uhalifu kwa kulipa fedha hizo baada ya kuagizwa na Trump kwa nini rais Trump asionekane kuwa naye ametenda uhalifu?     

Wakati huo huo aliyekuwa meneja wa kampeni ya uchaguzi kwa niaba ya rais Trump bwana Paul Manafort amepatikana na hatia katika mashtaka manane yanayohusiana na uhalifu wa kifedha. Maseneta wa chama cha Republican wametoa kauli za tahadhari juu ya watu hao waliokuwa wapambe wakubwa wa rais Trump. Seneta Lindsay Graham amesisitiza kwamba jambo la umuhimu mkubwa kabisa ni kuthibitsha iwapo waendesha kampeni wa rais Trump walishirikiana na Urusi wakati wa uchaguzi wa rais nchini Marekani. Paul Manafort, aliyeongoza kampeni ya Rais Donald Trump kwa miezi miwili mnamo mwaka 2016, anaweza kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu jela iwapo atahukumiwa katika kesi mbili zilizofunguliwa dhidi yake na serikali ya Marekani.

Meneja wa zamani wa kampeni ya uchaguzi kwa niaba ya rais Donald Trump, Paul ManafortPicha: picture alliance/AP Photo/A. Brandon

Mambo muhimu yaliyo sababisha kukamatwa kwake hadi kufunguliwa mashtaka kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2005, Paul Manafort mwanasheria wa jijini Washington mwenye uhusiano wa karibu na chama cha Republican atakumbukwa kwenye historia kuwa alikuwa na ushawishi mkubwa kwa niaba ya madikteta wa nchi za nje ikiwa ni pamoja na Ferdinand Marcos wa Ufilipino na aliyekuwa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mobutu Sese Seko.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/AFPE/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW