1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasemavyo wahariri wa Ujerumani

Admin.WagnerD3 Februari 2016

Matokeo ya kura ya kwanza ya maoni kwa wagombea wa urais nchini Marekani, majadiliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza na ziara ya waziri mkuu wa jimbo la Bavaria mjini Moscow katika magazeti ya Ujerumani.

Infografik Iowa Vorwahl 2016 Englisch

Mhariri wa gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger ameandika juu ya kura ya maoni iliyofanyika katika jimbo la Iowa siku ya Jumatatu, kuchagua wagombea watakaopeperusha bendera za vyama vya Republican na Democrats kwenye uchaguzi mkuu. Mhariri huyo anasema habari njema ni kuwa Donald Trump siyo mtu asiyeshindika. Makaripio yake hayakupata uungwaji mkono kama ilivyotarajiwa. Lakini habari mbaya ni kwamba mawazo ya Ted Cruz, mshindi wa kura hiyo ya kwanza ni hatari pia. Mgombea huyo kutoka Texas yuko katika vita vya kidini dhidi ya usasa.

Kwa upande wa pili, mhariri huyo anasema wafuasi wengi wa chama cha Democratic wameamua kukimbilia kwa Bernie Sanders na hawataki kujua chochote kuhusu siasa za mzoefu Hillary Clinton. Hii inatoa picha ya kuzidi kwa itikadi kali na kukosekana kwa maudhui katika mijadala ya kisiasa nchini Marekani.

Mhariri wa gazeti la Allgameine anasema uchaguzi huu unaonesha jinsi Marekani ilivyogawanyika kuliko ilivyowahi kutokea. Anasema taifa hilo limebanwa katikati ya kupotea kwa maana ya utandawazi na msimamo mikali inayochagizwa na miito ya kurudi kwenye misingi ya maadili yake. Maswali yote kuhusu Marekani ambayo siyo rahisi kupatiwa majibu, yanawatia hofu watu katika miji ya New York au Los Angeles, kama ilivyo kwingineko mfano Iowa. Na ndiyo maana dunia inasubiri kuona kitakachotokea.

Uingereza inataka mabadiliko katika Umoja wa Ulaya ili iendelee kuwa mwanachama wa umoja huo.Picha: picture-alliance/empics

EU inaihitaji Uingereza lakini...

Mhariri wa gazeti la Berliner Zeitung ameandika kuhusu majadiliano yanayoendelea kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, juu ya mabadiliko inayoyataka Uingereza yafanyike ili kuiepusha kuwa nchi ya kwanza kujitoa katika umoja huo. Mhariri huyo anasema:

Ulaya inaihitji Uingereza. Inahitaji ukarimu wa Uingereza, ushawishi wake katika nyanja ya sera ya kigeni, na hata ukalifu wa Uingereza katika siasa za Ulaya. Lakini waziri mkuu David Cameron hajakaribia bado lengo lake la kuibakiza Uingereza katika umoja huo bado. Cameron anaweza kupata ushindi mjini Brussels, lakini akashindwa pia katika kura ya maoni. Hiyo itakuwa masikitiko. Kidogo kwa Cameron lakini kwa Umoja wa Ulaya, ambao unakabiliwa na nyufa kubwa. Mustakabali wa umoja huo umegeuzwa kuwa mchezo wa wacheza kamari.

Horst Seehorfer ziarani Moscow

Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria na mshirika wa karibu wa Kansela Angela Merkel Hosrt Seehofer, anapanga kumtembelea rais wa Urusi Vladmir Putin hapo kesho, katika ziara iliyozuwa mjadala mkubwa hapa Ujerumani, kwa hofu kwamba inaweza kudhoofisha sera ya wakimbizi ya Kansela Angela Merkel. Juu ya ziara hii, mhariri wa gazeti la Thüringer Allgemeine ameandika:

Ni nadra kwa ziara ya kisiasa kusababisha kelele kubwa hata kabla haijaanza. Licha ya hayo Seehorfer ana haki kabisaa. Tumezungukwa na vyanzo vya moto wa kisiasa na vingi vinaweza angalau kutulizwa kwa msaada wa Putin.

Changamoto nyingi zinaweza kutatuliwa tu kwa kujadiliwa kwa ngazi ya juu. Katika mgogoro wa Ukraine hakuna kinachofanyika, nchini Syria Putin laazima asema anachotaka, na kwa changamoto ya kidiplomasia kuhusiana na msichana wa Berlin Lisa, ni bora kwa Moscow kuomba msamaha kwa manufaa yake.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef