1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel waonya juu ya nyuklia

12 Oktoba 2024

Viongozi wa shirika la Nihon Hidankyo la manusurura wa mabomu ya atomiki lililoshinda Tuzo ya Amani ya Nobel wametoa onyo kwamba hatari ya vita vya nyuklia inazidi kuongezeka.

Japan Hiroshima |
Toshiyuki Mimaki, Mwenyekiti mwenza wa kampuni ya Nihon Hidankyo iliyoshinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2024Picha: KYODO/REUTERS

Viongozi wa shirika la Nihon Hidankyo la manusurura wa mabomu ya atomiki lililoshinda Tuzo ya Amani ya Nobel, wametoa onyo mapema leo kwamba hatari ya vita vya nyuklia inazidi kuongezeka. Viongozi hao wametoa pia wito mpya wa kukomeshwa kwa silaha za nyuklia.

Mmoja wa walionusurika katika mashambulizi ya nyuklia yaliyofanywa na Marekani mwaka 1945 mjini Nagasaki, Shigemitsu Tanaka amesema hali ya kimataifa inazidi kuwa mbaya na sasa vita vinaendeshwa huku nchi zikitishia matumizi ya silaha za nyuklia.

Soma zaidi.Wajapani wapokea Tuzo ya Amani ya Nobel kwa machozi 

Wakati wa kutoa tuzo hiyo, Kamati ya Nobel ya Norway ilionyesha uharibifu uliotokana na milipuko ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki na kazi ya muda mrefu ya shirika hilo la Kijapani katika kutokomeza silaha za nyuklia duniani.

Tahadhari ya washindi hao wa tuzo ya amani ya Nobel imetolewa wiki kadhaa tangu Rais wa Urusi Vladimir Putin alipoashiria kuwa, Moscow itaangalia uwezekano wa kufanya mashambulizi ya nyuklia ikiwa Marekani na washirika wake watairuhusu Ukraine kushambulia ndani ya Urusi kwa makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na nchi za magaharibi kwa Ukraine.


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW