Washington. Benki kuu ya dunia kuiunga mkono taasisi itakayosimamia uhamishwaji wa mali kutoka kwa wayahudi kwenda kwa Wapalestina.
5 Mei 2005Benki kuu ya dunia iko tayari kuiunga mkono kwa muda taasisi ya Wapalestina itakayokuwa na jukumu la kuangalia uhamishwaji wa mali kwenda kwa Wapalestina mara tu Israel itakapoondoka kutoka katika maeneo ya ukanda wa Gaza.
Christian Poortman, makamu wa rais wa benki kuu ya dunia anayeshughulikia eneo la mashariki ya kati na Afrika ya kaskazini, amesema kuwa taasisi hiyo maalum itasaidia kuhakikisha kuwa nyumba za walowezi wa Kiyahudi katika eneo ukanda wa Gaza hazitavunjwa na kwamba Wapalestina hawatakimbilia kuingia katika nyumba hizo.
Poortman ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa benki hiyo iko tayari kuchukua jukumu la ushauri na kuwa mshirika katika zoezi hilo, lakini benki hiyo pia haiko tayari kununua mali hizo ama kuuza.
Israel imepanga kuwaondoa walowezi kutoka katika maeneo 21 katika ukanda wa Gaza na maeneo manne kutoka 120 katika ukingo wa magharibi mwaka huu chini ya mpango wa waziri mkuu Ariel Sharon wa kujiondoa kutoka katika mzozo na wapalestina.