WASHINGTON : Bush aionya Korea Kaskazini
21 Septemba 2007Rais George W. Bush wa Marekani ameionya Korea Kaskazini dhidi ya kuipatia Syria maarifa ya nuklea kwa kusema kwamba mazungumzo ya pande sita na serikali ya Korea Kaskazini yanaweza tu kufanikiwa iwapo itatimiza ahadi zake zote.
Hata hivyo duru mpya ya mazungumzo iliokuwa imepangwa kufanyika hapo Jumaatano iliahirishwa ghafla kutokana na kuwepo kwa repoti kwamba serikali ya Korea Kaskazini ilikuwa ikisaidia Syria kutengeneza silaha za nuklea.
Serikali zote mbili za Korea Kaskazini na ile ya Syria zimekanusha repoti hizo.Katika makubaliano ya kihistoria yaliofikiwa hapo mwezi wa Februari utawala wa kikomunisti wa Korea Kaskazini ulikubali kutokomeza mitambo yake yote ya nuklea na mipango ili badala yake nchi hiyo ipatiwe ridhaa za kidiplomasia nishati pamoja na msaada mwengine.