WASHINGTON : Korea Kaskazini yatakiwa kurudi kwenye mazungumzo ya nuklea
11 Juni 2005Rais George W Bush wa Marekani na Rais Roh Moo-hyun wa Korea Kusini wameitaka Korea Kaskazini kurudi kwenye mazungumzo juu ya mpango wake wa silaha za nuklea.
Baada ya mkutano kwenye Ikulu ya Marekani viongozi hao hawakuzipa uzito tafauti zao juu ya namna ya kulishughulikia tatizo hilo.Serikali ya Marekani inaunga mkono msimamo mkali katika kulishughulikia suala hilo na inataka kuiona Korea Kaskazini inachukuwa hatua kabla ya kuipatia manufaa ya kiuchumi.Korea Kaskazini inataka kulishughulikia suala hilo kwa njia ya maridhiano zaidi.
Korea Kaskazini hivi karibuni ilidokeza azma yake ya kurudi tena kwenye mazungumzo hayo yanayoshirikisha nchi sita ambayo ilijitowa mwaka mmoja uliopita lakini pia inaendelea kuzungumzia juu ya silaha zake za nuklea na shauku yake ya kutengeneza mabomu zaidi ya nuklea.