WASHINGTON
16 Februari 2005Serikali ya Marekani imemrejesha nyumbani balozi wake nchini Syria.Uamuzi huo umefuatia kuuawa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Harir,katika shambulio la bomu lililotegwa ndani ya gari mjini Beirut juzi siku ya Jumatatu.Watu wengine 17 pia waliuawa katika shambulio hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Richard Boucher amewambia waandishi wa habari mjini Washington,kuwa Balozi Margaret Scobey ameitwa nyumbani kwa kile alichokiita mashauriano ya dharura.
Wakati huo huo msemaji wa Ikulu ya Marekani amesema kuwa serikali ya Washington imekuwa katika mazungumzo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,kuhusiana na hatua za kuchukuliwa kwa wale wote waliohusika na mauaji ya Bwana Hariri.Hata hivyo bado haijajulikana ni akina nani wanahusika na shambulio la bomu lililomuua Bwana Hariri.
Nako nchini Lebanon kwenyewe,viongozi wa upinzani wameituhumu Syria kuwa inahusika na mauaji ya Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Lebanon,huku waombolezaji wakiwa wanawashambulia kwa mawe na bakora wafanyakazi raia wa Syria wanaofanya kazi katika mji aliozaliwa Bwana Hariri wa Sidon huku wakitoa kauli nzito za kumkashifu Rais wa Syria Bashar al Assad kutokana na mauaji hayo.Maandamano mengine makubwa yamefanyika katika mji wa bandari wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon kulaani mauaji ya Bwana Hariri.