WASHINGTON:Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lapitisha azimio juu ya Korea kaskazini
16 Julai 2006Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeidhinisha kwa pamoja azimio la vikwazo dhidi ya Korea kaskazini juu ya majabirio ya makombora yake hivi karibuni.
Hatua hiyo iliyokuwa inapigiwa upatu na Japan imefikiwa baada ya China kukubaliana nayo katika dakika za mwisho.
Mjumbe wa serikali ya mjini Pyongyang katika Umoja wa mataifa Pak Gil Yon amelaani hatua hiyo kwa kile alichokiita kuwa ni kitendo cha kuchukiza chenye malengo ya kisiasa kuishinikiza Korea Kaskazini.
Amesisitiza mjumbe huyo kuwa majaribio ya makombora ya Korea Kaszini yalikuwa ni utaratibu wa kawaida wa kijeshi kwa ajili ya malengo yake ya ulinzi na kuishutumu Marekani kwa usaliti.
Hata hivyo mjumbe huyo wa Pyongyang amesema licha ya kuidhinishwa azimio la kuiwekea vikwazo Korea kaskazini vya kuyajaribu makombora na kuipiga marufuku ya kufanya biashara ya bidhaa na technologia inayohusiana na silaha za maangamizi makubwa, nchi hiyo itaendelea kuyajaribu makombora yake.