1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washirika wa Marekani waungana kujibu vikwazo vya Trump

Daniel Gakuba
1 Juni 2018

Nchi washirika wa Marekani zimekasirishwa na hatua za serikali ya Rais Donald Trump kuziwekea vikwazo vya kiushuru, vinavyolenga bidhaa za chuma cha pua na bati. Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico, zimeapa kulipiza kisasi.

Stahlproduktion in Deutschland
Bidhaa za chuma cha pua na bati kutoka Ulaya, Canada na Mexico zimewekewa vikwazo vya ushuru ziingiapo MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Canada na Mexico zilitangaza mara moja hapo jana hatua za kujibu ushuru mpya uliowekwa na Marekani dhidi ya bidhaa zao za chuma cha pua na bati zinazoingizwa kwenye soko la nchi hiyo, nao Umoja wa Ulaya umesema tayari umejipanga kuujibu uamuzi huo wa serikali ya Trump. Waziri wa fedha wa Ujerumani Peter Altmeier amezungumzia uwezekani wa kushirikiana na Canada pamoja na Mexico, kuratibu mkakati wa pamoja dhidi ya Marekani.

Tangazo hapo jana kutoka kwa waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross la kuanzisha rasmi vikwazo vya kiushuru dhidi ya Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico lilihitimisha kipindi cha miezi kadhaa ya sintofahamu, juu ya iwapo Marekani ingeelea kuziondoa nchi hizo kwenye orodha yake ya vikwazo vya kibiashara.

Ulaya yakasirishwa

Katika hatua hizo, bidhaa zote za chuma cha pua  zinazoingizwa Marekani kutoka Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico ushuru wake umeongezwa kawa asilimia 25, na ongezeko la asilimia 10 limewekwa dhidi ya bidhaa za bati. Akizungumza mjini Brussels muda mfupi baada ya uamuzi wa Marekani, Rais wa kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker alionekana dhahiri kuchukizwa, aliulaani uamuzi huo.

Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker amesema Ulaya haitajikunyata mbele ya vikwazo vya MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/O. Matthys

''Hii ni siku mbaya kwa biashara ya dunia. Ulaya haiwezi kukaa kimya kuhusiana na hatua kama hizi. Tutafikisha mara moja malalamiko katika Shirika la Kimataifa la Biashara, na mnamo saa chache zijazo, tutaweka wazi mpango wetu wa kulipiza kisasi.'' Amesema Juncker na kuongeza kuwa inachoweza kukifanya Marekani dhidi ya Ulaya, Ulaya pia inaweza kukifanya dhidi ya Mareakni.

''Haikubaliki hata kidogo kwamba nchi moja inaweza kujichukulia hatua kivyake katika biashara ya kimataifa.'' Amelalamika Juncker.

Macron amponda Trump

Ikulu ya Ufaransa mjini Paris imesema Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron alizungumza na Rais Trump baada ya vikwazo hivyo kutangazwa, na kumweleza wazi kwamba kwa hatua hizo, Marekani imefanya makosa, na imevunja sheria. Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau pia amemkosoa vikali rais Trump, na tayari Canada imetangaza ushuru mpya kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 12.8. Mexico pia imebainisha kuwa itaziongezea ushuru bidhaa za kilimo kutoka Marekani katika mzozo huo.

Rais Donald Trump amewapuuza wanaokosoa sera zake za biasharaPicha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Upinzani dhidi ya vikwazo hivyo vya ushuru vilivyowekwa na utawala wa Trump haukuja tu kutoka nchi zilizolengwa, bali pia kutoka Marekani kwenyewe. Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Paul Ryan ambaye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa chama cha Republican anachotoka Trump, amesema hakubaliani na rais huyo.

Ryan amesema badala ya kuzilenga nchi washirika, utawala wa Trump ungekuwa unashirikiana nao kuibana China, ambayo amesema kwa maoni yake, ndio yenye matatizo. Trump amezipuuza kauli zote zinazomkosoa, akisema enzi za Marekani kudhulumiwa kibiashara zimefika kikomo.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema Marekani haiwezi kuepuka kuumizwa na hatua zake yenyewe. Baadhi ya athari zinazotabiriwa ni kupanda kwa bei za bidhaa zitokanazo na chuma cha pua  na bati, na kupotea kwa maelfu ya ajira.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre, ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW