Mazungumzo ya Paris juu ya Ukraine yakumbwa na sintofahamu
6 Januari 2026
Viongozi wa nchi rafiki wa Ukraine wamekutana Jumanne mjini Paris kwa mazungumzo muhimu yanayoweza kuamua mustakabali wa usalama wa Ukraine endapo makubaliano ya amani na Urusi yatafikiwa.
Hata hivyo, matarajio ya mafanikio yanaonekana kuwa dhaifu. Serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump imeelekeza nguvu zake kwenye masuala ya Venezuela, huku kauli za Marekani kuhusu uwezekano wa kudhibiti kisiwa cha Greenland zikizidisha mvutano kati ya Washington na Ulaya.
Kabla ya tukio la hivi karibuni linalohusisha Venezuela, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa ameonyesha matumaini juu ya mkutano wa kile kinachoitwa Muungano wa Walio Tayari, ambao kwa miezi kadhaa umekuwa ukijadili namna ya kuzuia Urusi kufanya mashambulizi mapya iwapo itakubali kusitisha vita.
Katika hotuba yake ya Desemba 31, Macron alisema washirika wa Ukraine wangetoa "ahadi za dhahiri” katika mkutano huo "kuilinda Ukraine na kuhakikisha amani ya haki na ya kudumu.”
Ofisi ya Macron imesema idadi isiyokuwa ya kawaida ya viongozi imehudhuria mkutano huo ana kwa ana, uliohudhuriwa na washiriki 35, wakiwemo wakuu 27 wa nchi na serikali.
Wajumbe wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, walikutana na Macron katika Ikulu ya Elysee kabla ya mkutano huo.
Msimamo wa Urusi na juhudi za kidiplomasia
Urusi imeendelea kutoweza wazi msimamo wake katika mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani. Maafisa wa Kremlin wamesisitiza kuwa hakuna usitishaji mapigano utakaokubaliwa bila makubaliano ya kina ya kisiasa.
Moscow pia imeweka wazi kuwa haitakubali kupelekwa kwa wanajeshi kutoka nchi za NATO kwenye ardhi ya Ukraine, jambo linalozidi kutatiza mazungumzo ya usalama.
Pembeni mwa mkutano huo, kulifanyika mikutano kadhaa iliyoonyesha ukubwa na ugumu wa juhudi za kidiplomasia zinazoendelea.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alikutana na Macron kabla ya mkutano mkuu. Viongozi wa kijeshi wa Ufaransa, Uingereza na Ukraine pia walifanya mazungumzo, yakihusisha kamanda mkuu wa NATO, Jenerali wa Marekani Alexus Grynkewich.
Mkutano na waandishi wa habari uliopangwa baadaye uliwakutanisha Zelenskiy, Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz.
Mvutano wa Greenland na mizani ya kidiplomasia
Mvutano uliongezeka baada ya Rais Trump kurejea miito yake ya Marekani kukidhibiti kisiwa cha Greenland, chenye rasilimali nyingi katika eneo la Aktiki.
Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Hispania na Uingereza walisimama pamoja na Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, kutetea mamlaka ya Greenland.
Hata hivyo, Ulaya bado inahitaji nguvu za kijeshi za Marekani ili kuunga mkono dhamana za usalama wa Ukraine na kuzuia tamaa za Urusi za kupanua maeneo yake.
Washiriki wa mkutano wanatafuta makubaliano juu ya vipaumbele vitano: ufuatiliaji wa usitishaji mapigano, msaada kwa jeshi la Ukraine, kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa ardhini, baharini na angani, hatua za kuchukua iwapo Urusi itashambulia tena, na ushirikiano wa muda mrefu wa ulinzi.
Lakini kufanikisha yote hayo bado ni jambo lisilo na uhakika, hasa baada ya operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela, iliyopelekea kutekwa kwa kiongozi wa taifa hilo Nicolas Maduro.
Ukraine yataka dhamana thabiti
Ukraine inataka dhamana thabiti kutoka Washington, ikiona hilo kuwa muhimu ili kupata ahadi sawa kutoka kwa washirika wengine. Kyiv ina hofu kuwa usitishaji mapigano bila ulinzi wa kutosha unaweza kuipa Urusi nafasi ya kujipanga upya.
Mjumbe wa Marekani Steve Witkoff ameashiria kuwepo kwa maendeleo katika mazungumzo ya hivi karibuni, akisema mjadala umejikita katika kuimarisha dhamana za usalama na kuweka mifumo ya kuzuia vita kurejea.
Ufaransa na Uingereza, ambazo zinaongoza juhudi za kijeshi za Ulaya, zimesema mstari wa kwanza wa ulinzi wa Ukraine utabaki kuwa jeshi lake lenyewe, huku likiungwa mkono kwa mafunzo, silaha na teknolojia.
Zelenskiy amesema bado kuna vikwazo katika kupelekwa kwa wanajeshi wa Ulaya, akisisitiza kuwa si kila nchi iko tayari kuchukua hatua hizo, jambo linaloibua maswali juu ya uimara wa Muungano wa Walio Tayari.
Wakati huo huo, mapigano yanaendelea. Ukraine imesema imeshambulia kwa droni ghala la silaha na bohari la mafuta ndani ya Urusi, hatua inayoonyesha kuwa licha ya juhudi za kidiplomasia, vita bado havijaisha.
Chanzo: APE, RTRE, AFPE, DPAE