1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washiriki 2,000 wahudhuria kongamano la wanahabari Bonn

20 Juni 2022

Kongamano la 15 la vyombo vya habari ulimwenguni limeanza hivi leo hapa mjini Bonn likiwa ni mara ya kwanza kwa washiriki kukusanyika pamoja tangu janga la virusi vya korona lianze ulimwenguni mwishoni mwa mwaka 2019.

Global Media Forum in Bonn | brasilianische Journalistin Patricia Toledo de Campos Mello
Picha: Guilherme Becker/DW

Kongamano hilo la siku mbili ambalo maudhui yake makuu ni KUIJENGA KESHO kwa kuanzia na leo, limefunguliwa rasmi katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa mjini Bonn mapema siku ya Jumatatu (20.06.2022).

Akifungua Kongamano hilo Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg, aligusia ugumu wa kazi ya uandishi wa habari katika zama hizi za janga la UVIKO-19 na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Washiriki zaidi ya 2,000 wa kongamano hili wameelezwa pia jinsi ukweli ulivyogeuka kuwa adui mkubwa mbele ya wenye mamlaka na makundi yenye nguvu ya kijamii, hali iliyomfanya mshindi wa mwaka 2021 wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Maria Ressa, kutoka Ufilipino kuishi kwa mashaka sehemu kubwa ya maisha yake ya kikazi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akihutubia kongamano hiloPicha: Ayse Tasci/DW

Kwenye kongamano la 2022, Maria Ressa alipewa nafasi ya kutoa hotuba kuu ya mjadala, chini ya kichwa cha habari: Je, uko tayari kujitolea kwa kiasi gani kwa ajili ya kusimamisha ukweli?:

Wazungumzaji wengine kwenye siku hii ya kwanza ya kongamano hili la siku mbili, ambalo linahudhuriwa na washiriki kutoka mataifa zaidi ya 100 duniani, walikuwa ni Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Bearbock, Waziri Mkuu wa Jimbo la Northrhine Westphalia unakofanyika mkutano huu, Hendrick Wüst, na Claudia Roth, waziri mwenye dhamana ya utamaduni na vyombo vya habari katika serikali kuu ya shirikisho la Ujerumani.Mkutano wa Jukwaa la vyombo vya habari DW waanza Bonn

Zaidi ya mada na warsha 40 zitaendeshwa kwenye kongamano hili la siku mbili, msisitizo ukiwekwa kwenye namna ambavyo taaluma ya uandishi wa habari inavyoweza kukabiliana na majaribu ya sasa katika ulimwengu uliojaa njia nyepesi na rahisi za kuwasiliana lakini zisizo za uhakika wala usimamizi.

Miongoni mwa taasisi za kimataifa zinazoshiriki moja kwa moja kwenye kongamano la mwaka huu ni Umoja wa Afrika, ambao umedhamini na kuendesha kikao maalum kilichopewa jina: Mustakabali wa Uandishi wa Habari barani Afrika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW